Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa wale wanaonufaika na ugaidi na wanaolenga kuutumbukiza ukanda huo katika machafuko na ukosefu wa utulivu watashindwa.
“Wafanyabiashara wa umwagaji damu watashindwa; watu wanaonufaika na ugaidi watashindwa. Wanaotekeleza mauaji ya halaiki wanaolenga kuutumbukiza ukanda wetu katika machafuko na ukosefu wa utulivu watashindwa,” Erdogan amesema Jumanne katika hafla ya kuadhimisha miaka 955 ya Vita vya Malazgirt, katika mkoa wa Bitlis, kusini-mashariki mwa Uturuki. Vita hivyo vilikuwa ushindi wa kihistoria kwa Waturuki katika eneo la Anatolia.
Rais Erdogan amesema dunia itashuhudia kuibuka kwa “Uturuki kubwa na yenye nguvu,” akiongeza kuwa mara tu mpango wa “Uturuki Isiyo na Ugaidi” utakapofikia lengo lake, “milango ya enzi mpya itafunguka mbele ya taifa letu.”
Ameongeza kuwa utu na udugu ndio vitashinda, pamoja na taifa la Uturuki na raia wake.
Akiashiria Ahlat, eneo muhimu lililokuwa sehemu ya mwanzo wa ushindi katika Vita vya Malazgirt (vinavyojulikana pia kama Vita vya Manzikert), Erdogan amesema: “Ushindi wa Yerusalemu na Istanbul unatokana na imani iliyojengeka huko Ahlat.”
“Msiruhusu mtu yeyote awe na shaka. Mapambazuko ya Uturuki kubwa na yenye nguvu yamewadia. Ujenzi wa ‘Karne ya Uturuki’ umeanza,” aliongeza.
Ushindi wa Waturuki katika Anatolia ulianza na Vita vya Malazgirt, vinavyojulikana pia kama Vita vya Manzikert, vilivyopiganwa Agosti 26, 1071. Katika vita hivyo, Waturuki wa Seljuk wakiongozwa na Sultan Alp Arslan waliishinda jeshi kubwa zaidi la Byzantine.
Ushindi huo uliharakisha kudorora kwa Dola ya Byzantine na kusababisha Waturuki wengi zaidi kuhamia katika eneo hilo, jambo lililoweka msingi wa kuibuka kwa Dola ya Ottoman na baadaye Jamhuri ya kisasa ya Uturuki.
Karne kadhaa baadaye, uvamizi wa vikosi vya kigeni uliichochea Uturuki kuanzisha Vita vya Uhuru mwaka 1919. Katika vita hivyo, vikosi vya Uturuki vilivyoongozwa na Mustafa Kemal Ataturk hatimaye viliwafurusha wavamizi kutoka Anatolia.
Kufikia mwishoni mwa mwaka 1922, vikosi vyote vya kigeni vilikuwa vimeondoka katika maeneo hayo, ambayo mwaka mmoja baadaye yakawa sehemu ya Jamhuri ya Uturuki.




















