| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Pakistan yalaani “jaribio la shambulio la droni” karibu na Makkah
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ameunga mkono Saudi Arabia baada ya mifumo yake ya ulinzi wa anga kuizuia droni karibu na mji mtakatifu wa Makkah, huku akitoa wito wa kujizuia kutokana na kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo.
Pakistan yalaani “jaribio la shambulio la droni” karibu na Makkah
Sharif alizitaka "pande zote" kujidhibiti na kujiepusha na hatua zinazoweza kuzidisha hali ya mzozo huo. / / Reuters

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, Jumatano amelaani vikali “jaribio la shambulio la droni” lililotokea karibu na mji mtakatifu wa Makkah nchini Saudi Arabia, na kuwataka wadau wote kufanya mazungumzo na kuepuka mzozo.

“Ninalaani jaribio hili la kikatili na la kutisha la kushambulia Eneo Takatifu la Makkah Al-Mukarramah,” Sharif amesema katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X.

Kwa mujibu wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo iliizuia na kuiharibu droni hiyo kabla haijaingia katika anga iliyofungwa karibu na Makkah. Waasi wa Houthi nchini Yemen, ambao Saudi Arabia iliwatuhumu kuhusika na shambulio la drone hiyo, walikanusha kuhusika na shambulio hilo.

Sharif atoa wito wa kusitishwa mapigano

Turki al-Malki, msemaji wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen, alisema droni hiyo ilidunguliwa majira ya saa 12:50 jioni kwa saa za GMT (takriban saa 9:50 usiku kwa saa za Saudi Arabia) siku ya Jumanne. Mabaki ya droni hiyo yalianguka kusini mwa Makka.

Sharif aliwataka “wahusika wote” kusitisha mapigano na kuchukua hatua za kuzuia hali isiendelee kuwa mbaya zaidi.

“Eneo letu tayari limeathirika sana kutokana na migogoro. Mazungumzo na diplomasia bado ndiyo njia pekee endelevu kuelekea amani,” alisema.

Waziri Mkuu huyo wa Pakistan pia amelisifu jeshi la Saudi Arabia kwa kile alichokiita umakini na weledi wa jeshi hilo, huku akithibitisha tena uungaji mkono wa Pakistana kwa mamlaka ya Saudi Arabia na usalama wa maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu yaliyoko Makkah na Madinah.

Kuimarika kwa ushirikiano wa ulinzi kati ya Pakistan na Saudi Arabia

Tukio hilo limetokea wakati Pakistan na Saudi Arabia zikiendelea kuimarisha ushirikiano wao katika masuala ya ulinzi.

Nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya ulinzi wa pamoja mwaka uliopita, na baadaye, mwezi Agosti, Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki zilitia saini mkataba wa pande tatu wa ushirikiano wa ulinzi mjini Makkah.

Sharif amesema Pakistan iko “bega kwa bega” na Saudi Arabia katika kulinda mamlaka yake pamoja na utakatifu wa miji miwili mitakatifu ya Makkah na Madinah.

 

CHANZO:TRT World and Agencies