Bunge la Libya siku ya Jumatatu liliidhinisha kwa pamoja makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa na Kamati Ndogo ya Majadiliano ya 4+4 yenye lengo la kuandaa mazingira ya uchaguzi wa urais na bunge, kulingana na taarifa ya bunge.
Msemaji wa Bunge Abdullah Bliheg anasema wabunge wameidhinisha kwa pamoja makubaliano hayo wakati wa kikao katika mji wa mashariki mwa nchi wa Benghazi.
Makubaliano hayo yanatoa nafasi ya kuundwa kwa Tume ya Uchaguzi, kuangazia masuala ya kisheria kwa uchaguzi wa urais na bunge, na kufanya uchaguzi huo chini ya mamlaka moja na taasisi za pamoja za kitaifa ndani ya muda wa miezi 24.
Utaratibu wa Uchaguzi
Makubaliano ya mwisho ya Kamati ya 4+4 yalitiwa saini Agosti 30 wakati wa hafla kwenye makao makuu ya UNSMIL mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Kamati hiyo inajumuisha wajumbe wanne wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli na wengine wanne kutoka mamlaka za mashariki mwa Libya.
Tarehe 3 Septemba, UNSMIL inasema iliwasilisha rasmi makubaliano hayo kwa Bunge na Baraza la Mawaziri, kuipa mihimili yote miwili mwezi mmoja kuidhinisha.
Raia wa Libya wanatarajia kuwa uchaguzi uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu utamaliza migogoro ya kisiasa na ile ya watu wenye silaha na kuondoa uongozi wa mpito ambao umeendela tangu kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi, ambaye aliongoza Libya kuanzia 1969 hadi 2011.




















