| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Shehena mpya ya vifaa vya kijeshi vya Marekani yawasili nchini Nigeria
Ndege ya kijeshi ya Marekani iliyobeba vifaa hivyo imewasili nchini Nigeria mwishoni mwa wiki, ikiwa ni sehemu ya mpango wa mauzo ya kijeshi kati ya Marekani na Nigeria.
Shehena mpya ya vifaa vya kijeshi vya Marekani yawasili nchini Nigeria
Kamandi ya Marekani barani Afrika ilisema kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya makubaliano ya mauzo ya kijeshi kwa nchi za nje. Picha: /USAfricaCommand

Kamandi ya Marekani barani Afrika (AFRICOM) imetangaza kusafirisha shehena mpya ya vifaa vya kijeshi nchini Nigeria.

AFRICOM imechapicha taarifa hiyo siku ya Alhamisi kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X, ikisema kuwa usafirishaji huo ni ishara nyingine ya kuimarika kwa ushirikiano wa kiusalama kati ya nchi hizo mbili.

Vifaa hivyo vilisafirishwa hadi Nigeria kwa kutumia ndege ya Jeshi la Anga la Marekani aina ya C-17 Globemaster III, chini ya mpango wa mauzo ya kijeshi (FMS) kati ya Marekani na Nigeria.

Vifaa hivyo, vilivyowasili mwishoni mwa wiki, vinatarajiwa kuimarisha uwezo wa Nigeria kukabiliana na ugaidi pamoja na vitisho vingine vya kiusalama.

Kuimarisha ushirikiano

AFRICOM ilisema mzigo huo umetolewa chini ya makubaliano ya mauzo ya kijeshi ya kigeni yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa ulinzi kati ya Marekani na Nigeria.

Uwasilishaji huo unafanyika wakati Nigeria ikiendelea kupambana na makundi ya kigaidi na waasi, huku ikiendelea na juhudi za kutafuta uungwaji mkono mkubwa zaidi wa kimataifa kwa ajili ya operesheni zake za kukabiliana na ugaidi.

Kutumika kwa ndege aina ya C-17 Globemaster III katika usafirishaji huu wa hivi karibuni kunaonyesha pia upande wa vifaa na usafirishaji wa ushirikiano huo, kwa kuwezesha vifaa vya kijeshi kusafirishwa moja kwa moja kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya ulinzi ya Nigeria.

AFRICOM haikutoa maelezo kuhusu aina ya vifaa vilivyowasilishwa wala thamani yake.

Uhusiano kati ya Marekani na Nigeria ulichukua mkondo mpya baada ya Rais Donald Trump kuiorodhesha tena Nigeria kama Nchi yenye Kutiliwa Mkazo Maalum.

Trump aliishutumu serikali ya Tinubu kwa kufumbia macho mauaji na kutishia kuishambulia Nigeria.

Hata hivyo, Serikali ya Nigeria ilituma ujumbe wa ngazi ya juu kwenda Marekani, na ujumbe kutoka Marekani nao ulitembelea Nigeria.

Marekani ilituma vikosi maalum nchini humo, na nchi zote mbili zikafanya operesheni maalum zilizolenga shabaha mahususi.

CHANZO:TRT Afrika and agencies