Mlipuko wa ugonjwa wa kimeta (anthrax) kaskazini mwa Zambia umesababisha vifo vya viboko 46, tembo wanane, nyati watano na mamba mmoja, huku watu 12 wakiambukizwa ugonjwa huo baada ya kula nyama kutoka kwenye mizoga ya wanyamapori iliyobainika kuwa na vimelea vya kimeta, kulingana na maafisa.
Watu walioambukizwa wanaendelea kupata matibabu huku serikali ikipeleka timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Munyamadzi na eneo la mto katika wilaya ya Mpika, mkoani Muchinga, ili kudhibiti mlipuko huo.
"Shughuli za uwindaji katika eneo lililoathirika zinapaswa kusimamishwa kwa muda hadi pale uchunguzi utakapobainisha hali ya ugonjwa huo na hatari zinazohusiana nao.’’ alisema Norman Chipakupaku, Mratibu wa Kitaifa wa Kitengo cha Kudhibiti na Kukabiliana na Majanga, katika taarifa yake siku ya Ijumaa.
Vifo vyovyote vya wanyama visivyojulikana chanzo chake vinapaswa kuripotiwa mara moja kwa mamlaka husika aliongeza Chipakupaku.
Chipakupaku aliongeza kuwa maafisa wa polisi wa wanyamapori na vituo vya ukaguzi vitaimarishwa ili kulinda maeneo yenye mizoga hiyo, kuzuia kusafirishwa na kuliwa kwa mizoga hiyo, pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji taarifa.
Pia aliwataka wananchi kutokula nyama ya wanyama waliokufa kiasili au kwa sababu zisizojulikana, na kuepuka kugusa mizoga ya wanyama.



















