Uturuki imewakamata washukiwa 175 katika msako kuhusu mtandao wa utapeli wa kimataifa ambao makampuni yake kwa sehemu kubwa yanamilikiwa au kusimamiwa na watu wenye uhusiano na Israel, Waziri wa Sheria Akin Gürlek alisema siku ya Ijumaa.
Gurlek anasema hayo yamebainika kutokana na uchunguzi mara nne mwaka huu wa Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka wa Istanbul kuhusu kampuni zinazoendesha vituo vya mawasiliano ambavyo vinatumia mitandao ya kijamii na matangazo mitandaoni kuwarubuni raia wa kigeni na ahadi za faida kubwa kwa biashara ya kuhawilisha fedha na uwekezaji.
Waziri huyo anasema uchunguzi ulibaini operesheni iliyolenga watu katika mataifa mbalimbali.
Faida za kupangwa, kurubuniwa kutoa fedha inatumika kuwatapeli watu
Kulingana na Gurlek, kuna wahudumu wanaozungumza lugha zaidi ya moja wanaowaleta watu wa kuwatapeli kwenye mfumo na kuwataka wawekeze kwenye maeneo kadhaa yanayodhibitiwa na washukiwa.
Wachunguzi walibaini majukwaa hayo yanadaiwa kuonesha faida zisizo za kweli kuwarubuni kuweka fedha nyingi. Wakati watu hao wanapotoa fedha wanaarifiwa kuwa wanahitaji kulipa zaidi kwa sababu zikiwemo vikwazo kwa akaunti na kodi.
Fedha hizo kisha zinatumwa kwa akaunti za benki na uwekezaji nje ya nchi, Gurlek anasema.
Uchunguzi huo uliratibiwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul kuhusu uchunguzi wa Uhalifu wa Ugaidi na Utakatishaji Fedha, kwa kushirikiana na Idara ya Ujasusi ya Uturuki (MIT), Idara ya Uhalifu wa Kupangwa na kitengo cha polisi cha Istanbul kinachofuatilia uhalifu wa mitandaoni.
Kitengo cha kukabiliana na utakatishaji fedha cha Uturuki MASAK kimetathmini fedha, intelijensia na uchunguzi wa polisi, pamoja na malalamiko kutoka kwa watu yaliyopatikana kupitia Interpol, kutumika katika uchunguzi, kulingana na Gurlek.
Msako ulifanyika katika maeneo 286 kwa wakati mmoja
Mamlaka zilianzisha operesheni ya pamoja saa kumi na moja alfajiri siku ya Ijumaa zikilenga makampuni 28, vituo 42 vya mawasiliano na washukiwa 239 katika sehemu 286 kote Istanbul na Mugla.
Kufikia saa nne asubuhi, mamlaka zilikuwa zimefika kwenye vituo vya mawasiliano na kuwakamata washukiwa 175, Gurlek amesema. Operesheni hiyo na juhudi za kuwakamata washukiwa zaidi zilikuwa zinaendelea.
Gurlek hakutoa maelezo zaidi kuhusu watu wanaohusishwa na Israel au kusema kama ni miongoni mwa waliokamatwa.






















