Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, amevienzi vizazi vya Wanamibia vilivyochangia katika mapambano ya ukombozi wa nchi hiyo, wakati mabaki ya mashujaa wanane yalipozikwa upya katika Makaburi ya Mashujaa, jijini Windhoek, Namibia.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Jumatatu, Nandi-Ndaitwah amewataja maveterani hao kuwa miongoni mwa waanzilishi wa mapambano ya ukombozi na wanachama waliojitolea wa SWAPO. Amesema wamejitolea maisha yao na kusaidia kuweka msingi wa uhuru ambao Namibia inaufurahia leo.
“Wajibu sasa uko kwa kizazi cha sasa kulinda na kujenga juu ya urithi huo,” alisema Nandi-Ndaitwah.
Rais huyo alisema kurejeshwa kwa mabaki ya mashujaa hao nchini Namibia ni hatua ya kurejesha heshima yao na kuwaunganisha tena na nchi yao.
Namibia na Afrika Kusini zilikamilisha mchakato wa kurejesha nchini mabaki hayo wakati wa hafla iliyofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini, siku ya Jumatano
Serikali za nchi hizo mbili zilisema zoezi hilo ni sehemu ya juhudi pana za Namibia na Afrika Kusini za kurejesha mabaki ya Wanamibia waliofariki au kuzikwa nje ya nchi wakati wa vipindi vya ukoloni na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Ushirikiano kati ya Namibia na Afrika Kusini
Katika hotuba yake, Nandi-Ndaitwah alimshukuru Waziri wa Ulinzi na Maveterani wa Afrika Kusini, Angelina Motshekga, kwa ushirikiano na msaada uliowezesha kukamilika kwa mchakato huo wa kurejesha mabaki.
Familia za maveterani hao wanane pia ziliwaenzi wanaume hao, ambao mchango wao na kujitolea kwao umetambuliwana kuheshimiwa katika Makaburi ya Mashujaa ‘Heroes' Acre’.
Mashujaa hao walitambuliwa kuwa Fillemon Nduuvu Nangolo, Festus Nehale, Immanuel Shifidi, Simon Petrus Niilenge, Eliaser Tuhadeleni, Immanuel Gottlieb Ndemulungila, Nathaniel Maxuilili, Tobias Hainyeko na Brendan Simbwaye.
Waziri wa Ulinzi na Maveterani wa Kijeshi wa Afrika Kusini, Angelina Motshekga, alizungumzia uhusiano wa karibu kati ya historia ya mapambano ya ukombozi ya Namibia na mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.
Akizungumza katika hafla ya kuwazika upya mashujaa hao, Motshekga alieleza gharama kubwa ya kibinadamu iliyolipwa katika mapambano ya ukombozi, ikiwa ni pamoja na miaka ya kuishi uhamishoni, kufungwa gerezani na kupoteza maisha mbali na nyumbani.
Alisema kurejeshwa kwa mabaki hayo kunawapa mashujaa waliofariki uhusiano wa mwisho na nchi ambayo walijitolea maisha yao kwa ajili yake. Pia, hatua hiyo inaziwezesha Namibia na Afrika Kusini kukabiliana na kukumbuka wakati mgumu ya historia yao ya pamoja.



















