Kwa miaka mingi, neno la mzee wa kimila katika jamii ya Kimasai ndilo lilikuwa la mwisho.
Leo, mmoja wa wazee hao anatumia mamlaka hiyo hiyo kuwaasa wenzake kuachana na baadhi ya mila katika jamii hizo.
Lungoviro Kivuyo ni mwenyeji wa Kijiji cha Pangaro, Kata ya Mgagao, Wilaya ya Mwanga-Kilimanjaro na Mwenyekiti wa viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Malaigwanani) wa Wilaya ya Mwanga.
Yeye mwenyewe, anakiri kuwa aliwahI kuwa sehemu ya mila kandamizi kwa wakati huo.
"Kila mila, hata inayokandamiza, niliiona sahihi" anasema na kuongeza:
"Awali, nilikuwa na msimamo mkali sana wa kulinda mila zetu za Kimasai," anasema Mzee Lungoviro.
Aliamini hakuna mila inayopaswa kuachwa au kuzuiwa, hata pale ambapo mila hiyo inawakandamiza wengine.
Anakiri pia kwamba alijua vitendo hivyo vinakiuka sheria za nchi, lakini akaviendeleza.
"Kuna wakati hata nyumbani kwangu nilikuwa naruhusu ukatili wa kijinsia kufanyika. Watoto kukeketwa na hata wanawake kupigwa. Sikujali kwamba ni kosa na tunatakiwa kuacha, licha ya kujua kwamba tunavunja sheria za nchi."
Mafunzo yaliyobadilisha msimamo
Mabadiliko yalianza baada ya mafunzo ya wazee wa mila kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, yaliyotolewa mwaka 2024 na 2025 na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kupitia mradi wa Porticus, uliolenga kuondoa vikwazo vya kufikia usawa wa kijinsia ikiwepo kutokomeza Ukatili wa Kijinsia.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha wazee wa mila kujadili masuala hayo kwa kina.
"Nilipopata mafunzo hasa yale ya wazee wa mila, ambapo TGNP walitupa nafasi ya kukutana na kujadiliana masuala haya kwa undani, niliamua kubadilika binafsi," anasema.
Aliweka msimamo wa kuwalinda watoto wa kike katika familia yake, pamoja na wake zake.
Midahalo ya wanaume: Mwanzo wa mabadiliko
Mbali na mafunzo hayo, Mzee Lungoviro anataja midahalo ya wanaume kuhusu ukatili wa kijinsia iliyofanyika vijijini kama sehemu muhimu ya safari yake.
Katika midahalo hiyo, wanaume hukutana wenyewe kwa wenyewe na kuzungumza wazi kuhusu jinsi ukatili unavyotokea majumbani, kwa nini unaendelea na madhara yake kwa familia nzima.
Midahalo hiyo iliwaweka pamoja wanaume, wazee wa mila wanaume na wazee maarufu vijijini.
Kulingana naye, midahalo hiyo ilimsaidia kujitazama upya kama baba na kama kiongozi, akawatazama watoto wake wa kike akatambua kwamba wanahitaji kulindwa dhidi ya ukatili.
Sasa anaitumia elimu hiyo kuwafikia wanaume wenzake.
Ujumbe unapotoka kwa mwanaume mwenzao, tena mzee wa mila anayeheshimika, huwa mzito na hausikiki kama shinikizo la kutoka nje.
Haya hivyo, anakiri kuwa bado kuna changamoto, akieleza kuwa, wapo wanaume ambao hawako tayari kubadilika, na baadhi yao huona mabadiliko haya kama udhalilishaji au kupokonywa nafasi yao ya uongozi katika ngazi ya kaya.
Hata hivyo, anasema wataendelea kuzungumza nao polepole.
Akiwa kiongozi wa Malaigwanani wa wilaya nzima ya Mwanga, Mzee Lungoviro ameamua kuiingiza ajenda ya ukatili wa kijinsia kwenye vikao vya viongozi wa kimila, hasa ukeketaji wa wasichana, ndoa za utotoni na kipigo kwa wanawake, mambo ambayo yamekuwa ya kawaida katika jamii ya Kimasai.
"Kwa kutumia nafasi yangu ya kiongozi wa kimila, hakuna mahali ninaposimama kuzungumza bila kuchomekea ajenda hizo," anasema.
Matokeo yake ni makubaliano miongoni mwa wazee. Sherehe za kimila za kuwavusha vijana wa kiume na wa kike rika zitaendelea, lakini bila ukeketaji.
"Kwa watoto wa kike, nimewaambia wenzangu tubadilishe mfumo huu, tuache ukeketaji. Tutawafanyia sherehe, vijana watakula na kunywa, na watapewa mafunzo ya kukua na kuvuka rika, lakini hatutowakeketa."
Wanawake wapewa nafasi
Pamoja na kuacha vitendo vya ukatili, wazee hao wamekubaliana kuwapa wanawake nafasi ya kupata elimu, kushiriki katika vikundi na kufanya shughuli za kiuchumi.
Mzee Lungoviro anamtaja Oliver, mwanamke wa Kimasai na katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) cha Kata ya Mgagao, kuwa mfano wa mabadiliko haya.
Leo sauti yake inasikilizwa mbele ya watu mbalimbali, jambo ambalo awali lisingewezekana.
Kuhusu kuchapa wanawake fimbo, anasema hakuna mzaha.
"Ulikuwa ukatili mkubwa, wanawake walichapwa bila huruma na hawakuwa na uwezo wa kujitetea."
Anakiri kwamba mila hii bado inaendelea katika jamii ya Kimasai, na kwamba bado kuna kazi ya kufanya.
Vijana wapokea kijiti
Mabadiliko haya hayaishii kwa wazee. Lazaro Kipuyo, kijana wa Kimasai, anasema elimu waliyopewa wazee wa mila imewasaidia sana kubadilika.
"Wazee wetu ndio kila kitu. Wakishabadilika hawa, hakuna shida tena. Sasa hivi sisi vijana wa kiume tuliopata elimu hii ya TGNP tumepata nguvu ya kuanza kuitoa elimu kwa nguvu zaidi."
Kwa Mzee Lungoviro, funzo ni rahisi: mila si mzigo wa kubeba milele, bali ni maisha ya jamii yanayoweza kuboreshwa.
Sherehe zitaendelea, na kilichobadilika ni kwamba mtoto wa kike atavuka rika akiwa mzima na salama.
Sheria iko upande wa mabadiliko
Kinachofanywa Mgagao kinaendana na mfumo wa kisheria wa Tanzania.
Ukeketaji ni kosa la jinai chini ya Kifungu cha 169A cha Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16), kilichoongezwa na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998.
Kifungu hicho kinamwadhibu mtu mwenye jukumu la malezi ya mtoto aliye chini ya miaka 18 anayesababisha akeketwe, kwa kifungo cha miaka mitano hadi kumi na tano jela, faini, au vyote viwili.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 nayo inamlinda mtoto dhidi ya ukatili na mila zinazohatarisha ustawi wake.
Kuhusu ndoa za utotoni, katika kesi ya Rebeca Gyumi, Mahakama Kuu (2016) na Mahakama ya Rufani (2019) zilibatilisha vifungu vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 vinavyomruhusu msichana kuolewa akiwa na umri mdogo kuliko mvulana, na kuitaka Serikali kurekebisha sheria ili umri wa chini uwe miaka 18.
Kwa upande wa kipigo, Kanuni ya Adhabu inatambua kushambulia na kujeruhi kuwa makosa ya jinai, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano (Ibara ya 12 na 13) inasisitiza utu, usawa na ulinzi dhidi ya vitendo vya kikatili na vya udhalilishaji.
Kwa upande wa sera, Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA) unasisitiza kuwahusisha viongozi wa kimila na kidini pamoja na wanaume katika mapambano haya.
Tanzania pia imeridhia Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake barani Afrika, inayokataza ukeketaji.
Kwa maneno mengine, uamuzi wa Mzee Lungoviro na wenzake haupingani na mila zao halisi, bali unaipa jamii nafasi ya kuishi ndani ya sheria za nchi.



















