Wizara ya Mambo ya Nje ya China imethibitisha kuwa Rais wa China, Xi Jinping, atafanya mkutano na Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, baadaye wiki hii.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara hiyo, Xi, Putin na Trump watakutana siku ya Alhamisi katika jiji la Shenzhen, lililoko kusini mwa China, pembezoni mwa Mkutano wa 33 wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC).
Ingawa wizara ya China haikutoa ufafanuzi kuhusu ajenda mahususi ya mazungumzo hayo, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alithibitisha siku ya Jumamosi kuwa mkutano huo umepangwa kufanyika Alhamisi. Uthibitisho huo ulifuatia taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House siku ya Ijumaa.
Kupunguza silaha za nyuklia
Akieleza vipaumbele vya Marekani kabla ya mazungumzo hayo, Msaidizi wa Katibu wa Habari wa White House, Olivia Wales, aliwaambia waandishi wa habari katika mazungumzo kwa njia ya simu kuwa udhibiti wa silaha utakuwa miongoni mwa masuala yatakayopewa uzito mkubwa katika majadiliano hayo.
"Miongoni mwa masuala mengine, atajadili upunguzaji wa silaha za nyuklia duniani, ambazo Rais Trump anaamini kuwa kuenea kwake ni hatari sana," alisema Wales.
Wales aliongeza kuwa, kabla ya kushiriki katika mkutano huo wa pande tatu, Trump atafanya mkutano rasmi na Xi pamoja na kushiriki chakula cha mchana siku ya Alhamisi alasiri. Baada ya hapo, atahitimisha ziara yake rasmi nchini China kwa kuhudhuria mkutano wa viongozi hao watatu.
Mkutano wa viongozi wa APEC umepangwa kufanyika kuanzia Novemba 18 hadi 19.
Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa mkutano huo wa pande tatu, mshauri wa kidiplomasia wa Kremlin, Yury Ushakov, alithibitisha mwezi uliopita kuwa Mareakni na Urusi bado hazijakamilisha mipango ya kufanyika kwa mkutano mwingine wa moja kwa moja kati ya Putin na Trump, pembeni mwa mkutano huo.





















