Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa atasimamisha operesheni ya kijeshi ya Marekani ya kusindikiza meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz , ikiwa ni juhudi ya kufikia makubaliano na Iran ili kumaliza vita vya Mashariki ya Kati.
“Project Freedom (Usindikizaji wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz) itasitishwa kwa muda mfupi ili kuona kama Makubaliano yanaweza kukamilishwa na kusainiwa,” Trump alisema kwenye mtandao wake wa Truth Social.
Akiashiria kupokea maombi kutoka Pakistan na nchi nyingine, pamoja na hatua iliyopigwa kuelekea makubaliano ya mwisho na Iran, lakini akasisitiza kuwa mzingiro wa majini utaendelea kutekelezwa kikamilifu.
Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema kuwa awamu ya mapigano ya operesheni za Marekani zilizoanzishwa dhidi ya Iran mwezi Februari imekamilika, na kwamba Marekani sasa inalenga operesheni mpya ya kuelekeza meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Makubaliano yanayoweza kufikiwa na Iran
“Project Freedom” ilitangazwa na Donald Trump siku ya Jumatatu, na operesheni hiyo ilitarajiwa kusaidia kuelekeza meli kutoka nchi ambazo hazihusiki na vita dhidi ya Iran kupita salama katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Ikitekelezwa na Kamandi Kuu ya Marekani, operesheni hiyo ilihusisha manowari zenye makombora elekezi, zaidi ya ndege 100, mifumo isiyo na rubani, na maelfu ya wanajeshi waliotoa mwongozo, msaada wa kuepuka mabomu ya baharini, na utayari wa kujilinda kwa meli za kibiashara bila kusindikizwa kikamilifu.
Mpango huo ulikuwa na lengo la kukabiliana na vizuizi vya Iran vilivyokuwa vinavuruga mtiririko wa mafuta duniani, na uliwasilishwa kama juhudi ndogo ya kujihami, ikilenga uhuru wa usafiri wa majini na kulinda meli zisizo na hatia.
Operesheni hizo zilishuhudia mvutano wa awali uliosababisha makabiliano, lakini sasa zimesitishwa ili kuendeleza juhudi za kidiplomasia kuelekea makubaliano yanayoweza kufikiwa na Iran.
















