Swala Bongo wa milimani wenye asili ya Kenya
Swala bongo wa milimani / Reuters
Swala Bongo wa milimani wenye asili ya Kenya
Swala wa Bongo wa milimani asili yake ni misitu ya milima mirefu ya Kenya, na inakadiriwa kuwa, wanyama hao wapo kati ya 100-140 katika pori nchini Kenya.

Kenya hivi majuzi ilisherehekea kupokea aina ya swala adimu, maarufu kama Mountain Bongos.

Swala wanne waliwasili nchini humo baada ya miaka mingi ya kuwa chini ya uangalizi katika bustani ya wanyama iliyopo Jamhuri ya Czech.

Lakini kwa nini swala hawa wanathaminiwa sana?

Swala wa Bongo wa Milimani asili yake ni misitu ya milima mirefu ya Kenya, na inakadiriwa kuwa, wanyama hao wapo kati ya 100-140 katika pori nchini Kenya.

Hii inamaanisha kuwa hawapatikani mahali pengine popote duniani katika mazingra yao ya asili isipokuwa nchini Kenya.

Ni mojawapo ya swala wakubwa wa msituni, wenye ngozi nyekundu-kahawia, wakiwa na alama nyeusi, nyeupe na njano-nyeupe.

Swala majike na madume wote wana pembe ndefu, zilizopinda kiasi.

Swala wa Bongo wa milimani ni nadra kuonekana katika makundi makubwa.

Fahali wengi hukaa peke yao, huku majike wakiwa na watoto wachanga hukaa katika makundi madogo ya hadi wanyama 10.

Wanyama hawa, wanapenda kutembea usiku.

Wanapatikana  katika misitu ya milimani ya nyanda za juu za Kenya, ikiwa ni pamoja na Aberdares na Mlima Kenya.

Huduma ya Wanyapori nchini Kenya inasema kuwa kwa sasa kuna jumla ya swala swala 106 katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Mlima Kenya (MKWC).

Chakula chao kikubwa ni majani, zabibu, magome ya miti na mara kwa mara nyasi.

Mara nyingi wanakuwa katika maeneo ya maji yenye madini wakiramba chumvi.

Hawa ndio swala wakubwa na wazito zaidi Afrika wakiwa na urefu wa sentimita 128. Madume wana uzito wa kilo 405 na majike wanafikia hadi kilo 253.

Majike huzaa ndama mmoja karibu miezi tisa baada ya kupata mimba.

Wanawaficha ndama wao kwenye mimea ili kuwalinda dhidi ya wanyama wanaowinda wanyama wengine, wakirudi mara kwa mara kuwanyonyesha, na ndama huachishwa kunyonya wakiwa na miezi sita hivi.

Lakini kwa wachache tu waliobaki, wapo hatarini kutoweka.

Wataalamu wanasema upotevu mkubwa wa makazi, ujangili, na magonjwa vinachangia kuwaangamiza.

Swala hawa wakubwa wa msituni pia wameteseka kutokana na upanuzi shughuli za kilimo, ukataji miti, na uwindaji haramu.