Shambulio la usiku la wanaoshukiwa kuwa magaidi wa Boko Haram katika kambi ya jeshi ya Chad limewaua watu wasiopungua 24, afisa mmoja wa jeshi na msimamizi wa kanda waliiambia AFP siku ya Jumanne.
Kambi ya Barka Tolorom iko ufukweni mwa Ziwa Chad, ambalo limesambaa Cameroon, Chad, Niger na Nigeria.
Shambulizi hilo siku ya Jumatatu jioni "lilisababisha vifo vya watu 25 na kuwajeruhi wengine 46 kwa upande wa jeshi la Chad," chanzo cha jeshi kiliiambia AFP.
Afisa msimamizi alitoa idadi kuwa "24 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa."
'Shambulio la kikatili'
Wote walilitaja shambulio kuwa la Boko Haram, huku msimamizi akisisitiza kuwa "hali sasa iko shwari."
"Kwa mara nyingine, kundi la kigaidi la Boko Haram limefanya shambulio la kikatili usiku wa jana katika kambi yetu ya jeshi huko Barka Tolorom," Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno alisema siku ya Jumanne katika mtandao wa Facebook.
"Tutaendelea kupambana kwa njia thabiti zaidi hadi pale tishio hili litakapoisha," aliahidi, akitoa salamu zake za rambirambi kwa familia zilizofiwa.
Wanajeshi wamekuwa wakishambuliwa na magaidi wa Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad, huku shambulio la mwezi Oktoba 2024 likisababisha vifo vya wanajeshi 40 wa Chad.
















