Rais Jose Maria Neves wa Cape Verde ametangaza nia yake ya kuwania uongozi wa nchi hiyo, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Taifa hilo, linalopatikana katika bahari ya Atlantiki, linatarajiwa kufanya uchaguzi wake, Novemba 15, mwaka huu.
Neves, mwenye umri wa miaka 66, amewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, kati ya mwaka 2001 hadi 2016, kabla ya kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo mwaka 2021.
Uamuzi huo, sasa utamlazimu rais wa bunge la Cape Verde, Janira Hopffer Almada, kushika wadhifa wa kaimu rais kwa kipindi cha miezi miwili ijayo.
"Kutokana na uzoefu wangu wa uongozi, nimeamua kuwania tena nafasi ya Urais, nikiwa na nia ya kutimiza malengo ya taifa letu,” alisema Neves, siku ya Jumatatu.
Hadi kufikia sasa, watu tisa wameweka wazi nia zao ya kuwania uongozi wa juu wa taifa hilo, huku wakisubiriwa kuwasilisha nyaraka zao katika mahakama ya katiba ya nchi hiyo, ifikapo siku ya Jumatano.
















