Nigeria imetwaa Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake la U-17 baada ya kuifunga Japan mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika Rabat, Morocco, na hivyo kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kushinda taji hilo.
Awawu Bashiru na Oluebube Umejiaku walifunga mabao hayo ya kihistoria kwa timu ya 'Flamingos' katika mchezo huo wa kusisimua uliofanyika Jumamosi jioni. Rais Bola Tinubu ameipongeza timu hiyo.
"Wasichana wetu wadogo wameuteka ulimwengu na kuwapa Wanigeria popote walipo sababu nyingine ya kusherehekea nchi yetu tukufu," alinukuliwa Rais Tinubu akisema katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bayo Onanuga.
“Ushindi wenu ni chachu kwa mamilioni ya wasichana wadogo wa Nigeria ambao wana ndoto ya kufikia mambo makubwa. Mmewaonyesha kuwa kwa kufanya kazi kwa bidii, kupata fursa na kuwa na azimio, wao pia wanaweza kufikia viwango vya juu zaidi vya mafanikio,” alisema Tinubu.
Ushindi huu wa kihistoria si wa Nigeria pekee, kwani timu ya 'Flamingos' ndiyo timu ya kwanza kabisa kutoka Afrika kushinda taji hilo. Nigeria iliishangaza Brazil katika hatua ya nusu fainali, kwa ushindi wa 3-1 siku ya Jumatano, na hivyo kufuzu kwa mchezo wa fainali.
Mafanikio bora zaidi ya awali kwa Afrika yalikuwa ni kushika nafasi ya tatu kwa Ghana mwaka 2012, na vilevile kwa Nigeria mwaka 2022; katika matukio yote mawili, timu hizo ziliifunga Ujerumani katika mechi za kuwania medali ya shaba.



















