| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Rais Erdogan anatarajiwa kuzuru Azerbaijan kwa Sikukuu ya Ushindi, asisitiza undugu 'thabiti'
Rais wa Uturuki anasema anatarajiwa kuwa kuwepo kwa sherehe za Novemba 8 jijini Baku, ni ishara ya historia ya pamoja, utamaduni na uhusiano wa karibu wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Rais Erdogan anatarajiwa kuzuru Azerbaijan kwa Sikukuu ya Ushindi, asisitiza undugu 'thabiti'
Rais Erdogan akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege akiwa njiani kutoka Korea Kusini Novemba 5 2026. (Ofisi ya Rais wa Uturuki) / Ofisi ya

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema anapanga kutembelea Azerbaijan tarehe 8 Novemba kuhudhuria sherehe ya Sikukuu ya Ushindi, akisisitiza umuhimu wa uhusiano kati ya Uturuki na Azerbaijan.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege kurudi kutoka Korea Kusini siku ya Jumanne, Erdogan alisema kuwa anatarajia kwenda Azerbaijan labda kuwe na sababu zisizoweza kuepukika kwa yeye kutotimiza safari hiyo.

Alisema amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev na pia amemtuma mkuu wa ujasusi wa Uturuki na waziri wa mambo ya nje jijini Baku kama sehemu ya mashauriano ya kidiplomasia yanayoendelea.

Erdogan aliongeza kuwa mawasiliano kati ya mataifa hayo mawili yameendelea, ikiwemo mazungumzo kati ya marais hao wawili na wake zao.

"Uhusiano wetu na Azerbaijan ni zaidi ya mawasiliano ya kidiplomasia," alisema, akieleza kuwa mshikamano wa nchi hizo msingi wake ni historia ya pamoja, utamaduni, na mustakabali.

"Hakuna kikwazo ambacho undugu wa Uturuki na Azerbaijan hauwezi kukabiliana nacho," aliongeza.

Sikukuu ya Ushindi ishara ya historia ya pamoja

Azerbaijan inaadhimisha Sikukuu ya Ushindi tarehe 8 Novemba, ikisherehekea ushindi wake katika vita vya Karabakh mwaka 2020.

Erdogan anasema siku hiyo ilikuwa muhimu kwa Azerbaijan na kueleza nia yake ya kuwepo kwenye sherehe hizo jijini Baku.

Haya yanadhihirisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili na umuhimu ambao Uturuki unauzingatia kwa kuendeleza ushirikiano wa karibu na mshirika wake.

Uturuki inataka kuimarisha uhusiano na Korea Kusini

Erdogan pia alijadili matokeo ya ziara yake ya Korea Kusini, akisema kuwa nchi zote zimesisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati.

Alisema biashara ya pamoja imepita zaidi ya Dola bilioni 11 na kwamba pande zote mbili zinalenga kuimarisha zaidi hadi Dola bilioni 15. Majadiliano kuhusu kuimarisha makubaliano yao ya biashara huria yanaendelea.

Rais anasema Uturuki na Korea Kusini wamekubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano katika nishati ya nyuklia, huku ufadhili ukiwa miongoni mwa masuala ambayo bado yanaendelea kujadiliwa.

Pia alieleza kuhusu uwezekano wa ushirikiano katika sekta ya ulinzi, ikiwemo miradi inayohusisha kifaru cha Altay, Firtina howitzers, droni, mifumo ya ulinzi wa angani na nyambizi. 

Makubaliano matano yanayohusisha nishati, madini, ushirikiano wa kisayansi, ufadhili wa miradi na uwekezaji yalitiwa saini wakati wa ziara hiyo.

Erdogan ataka kukutana na Putin baada ya mazungumzo na Zelenskyy

Kuhusu vita kati ya Urusi na Ukraine, Erdogan anasema ana nia ya kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin kufuatia mkutano wake wa hivi karibuni na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy nchini Uturuki.

Alisema Uturuki iliendelea kuunga mkono juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kumaliza vita hivyo na alitaka kujadiliana na upande wa Urusi kuhusu mchakato huo na Putin.

Erdogan aliongeza kuwa maafisa wa Uturuki, ikiwemo waziri wa mambo ya nje, wataendelea kuwasiliana na wenzao wa Urusi kujiandaa kwa majadiliano hayo.

Kuhusu uchaguzi wa nusu muhula wa Marekani, Erdogan alisema ilikuwa mapema kuzungumzia kwa ukamilifu kuhusu athari yake kwa uhusiano wa Uturuki na Marekani au sera ya Marekani ya Mashariki ya Kati.

Alisema Uturuki itaendelea na majadiliano na serikali ya Trump na mabunge yote mawili, akieleza matumaini kuwa matokeo hayo yatachangia katika amani ya kudumu na usalama kwenye kanda.

CHANZO:TRT World