Uturuki imekanusha madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii yanayodai kuwa huenda kukatokea shambulio la kigaidi jijini Ankara wakati wa mkutano wa NATO, ikiyataja madai hayo kuwa ni upotoshaji wa wazi na mbinu za kueneza hofu na taharuki.
Kituo cha Kupambana na Upotoshaji wa Taarifa kilichoko chini ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki kilisema katika taarifa iliyotolewa Ijumaa kuwa madai yanayosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii yanalenga kueneza hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.
Kituo hicho kilieleza kuwa madai hayo yamekusudiwa kuongeza wasiwasi na kudhoofisha imani ya umma kuhusu hali ya usalama.
"Hatua zote muhimu zimetekelezwa"
"Kila hatua muhimu ya usalama inatekelezwa kwa umakini mkubwa na taasisi husika," kituo hicho kilisema, kikiongeza kuwa hatua za kisheria pia zinaendelea dhidi ya wanaosambaza maudhui yenye nia ovu yanayotishia amani ya umma na usalama.
Kituo hicho kiliwasihi wananchi kufuatili taarifa zinazotolewa na mamlaka rasmi pekee na kupuuza madai yanayolenga kupotosha na kuchochea.
Uturuki itakuwa mwenyeji wa mkutano wa NATO tarehe 7–8 Julai, ambapo viongozi wa nchi wanachama watakutana kujadili uwekezaji katika ulinzi na sekta ya viwanda vya kijeshi, kuendelea kwa msaada kwa Ukraine, pamoja na mjadala mpana kuhusu ajenda ya NATO 3.0.














