Rais Donald Trump wa Marekani, amesema kuwa vita dhidi ya Iran bado havijaisha, akisisitiza nia ya kuushambulia mtambo wa ardhini wa nyuklia uliopo katika eneo la kusini la jiji la Tehran.
Eneo hilo, linalofahamika zaidi kama ‘Pickaxe Mountain’, lipo karibu na kinu cha nyuklia katika eneo la Natanz, ambapo mashushushu wa magharibi wanaamini kuwa linatumiwa na Iran, kujenga mtambo mwingine wa nyuklia.
"Tutalishambulia vikali eneo hilo katika siku za karibuni na hakuna lolote ambalo watafanya," alisema Trump siku ya Jumanne.
Kulingana na Trump ambaye alikuwa akizungumza na wanahabari mara baada ya kukutana na Rais Joseph Aoun wa Lebanon, itachukua zaidi ya miaka 20 kwa Iran kujijenga upya.
"Tukisema tuache vita leo, basi itawachukua Iran kati ya miaka 20 hadi 25, kujijenga upya. Na hivyo bado hatujamalizana nao kabisa."
Siku ya Jumanne, Iran iliongeza mashambulizi yake katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa ni wiki mbili toka kuanza kwa vita vyake na Marekani.












