Watu kumi na tatu ikiwemo maafisa watatu wa jeshi walifariki siku ya Ijumaa wakati ndege ya kijeshi ilipopata ajali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, afisa mmoja alisema.
Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea mji mkuu, Kinshasa, kutoka mji wa kusini magharibi wa Kikwit wakati ilipokuwa na tatizo la kiufundi na kujaribu kutua eneo la Kenge, mkoa wa Kwango, alisema Remy Saki Bokinda, makamu gavana wa Kwango.
"Kwa kuwa hakukuwa na sehemu ya kutua ndege eneo la Kenge, ndege iliingia katika sehemu ya makazi ya watu," alisema.
Miongoni mwa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo ni Jenerali Likulia Bakumi, mkaguzi mkuu wa hesabu za jeshi, pamoja na meja, kapteni na wanajeshi wengine na raia, Bokinda alisema.
"Wote waliokuwemo kwenye ndege walifariki; 12 waliungua kiasi cha kutotambulika, huku mwili wa rubani ukipatikana nje ya ndege," alisema.
Mamlaka ya anga ya DRC imeanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo, taarifa ya serikali ilisema.



















