Mariam Mwinyi ni mke wa Rais wa Zanzibar. Nafasi yake kama mke wa Rais wa Zanzibar ilianza mwaka 2020 wakati mumewe Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alipochaguliwa kuwa rais wa kisiwa hicho.
Mwinyi ni mtoto wa Rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Mariam alimaliza masomo yake ya juu ya sekondari nchini Tanzania kabla ya kuendelea na mafunzo ya udaktari na shahada ya uzamili nchini Uingereza.
Mariam na Mwinyi walioana miaka ya 1990 kabla ya Mwinyi kuwa Rais na hapo utaratibu wa Mariam ukabadilika akijitolea zaidi kwa maendeleo na ustawi wa jamii.
Kufuatia kuchaguliwa kwa Rais Mwinyi mwaka 2020, Mariam alianzisha miradi ya kusaidia jamii visiwani Zanzibar.
Mwaka 2021, alianzisha taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) na ameibuka kuwa mmoja wa wawezeshaji muhimu wa wanawake Zanzibar, pamoja na ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.
Kazi yake inajumuisha kutoa elimu na suluhu kwa kutumia mikakati ya kuimarisha maisha ya wanawake, watoto na jamii zilizo katika hatari.
ZMBF ina dhamira ya kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Kwa kuzingatia sera ya Uchumi wa Bluu ya Zanzibar, shirika hilo linazingatia sekta zinazofungamana kwa karibu na maisha ya wanawake.
Moja ya vipaumbele vyake vikuu ni kilimo cha mwani, sekta iliyo na idadi kubwa ya wanawake na kuaminika kuwa uti wa mgongo wa kaya nyingi za pwani.
Taasisi hiyo imesaidia kupatikana kwa nafasi za kazi katika sekta ya afya, elimu na usawa wa kijinsia.
ZMBF imekuwa ikishiriki kikamilifu katika miradi ya afya ya uzazi na mtoto, kampeni dhidi ya ukatili wa kijinsia na mipango inayolenga kulinda ustawi wa wasichana.
Mbali na majukumu ya ndani ya kisiwa hicho, Mariam Mwinyi pia hupata fursa ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa katika hafla mbali mbali.









