Sasa hivi mwanariadha wa Kenya wa mbio za marathon Sabastian Sawe ndiyo haabri ya mjini. Bingwa huyo siyo tu ameweka rekodi ya dunia lakini pia ameweka historia kwa kumaliza chini ya muda wa saa mbili.
Yaani alimaliza mbio za marathon za London katika muda wa 1:59:30 hiyo ni baada ya kukimbia kilomita 42.
Sabastian Kimaru Sawe alizaliwa miaka 31 iliopita, katika eneo maarufu kwa kutoa wanariadha walioelekea kuweka historia ulimwenguni.
Kuanza kwake riadha alikuwa zaidi katika mbio za masafa ya kati, hadi 2019 ambapo haikuwa kwa matakwa yake, lakini akajaribu mita 5,000 kutokana na kuchelewa kukosa nafasi kwenye mbio zingine. Aliibuka kidedea.
Kuanzia wakati huo akaanza kufanya mazoezi ya mbio ndefu. Alimaliza nusu marathon yake ya kwanza Januari 2022 katika muda wa dakika 59:02.
Mwezi wa tatu mwaka huo huo akaweka rekodi ya mbio za nusu marathon za Rome-Ostia akimaliza katika muda wa 58:58
Disemba 1 2024 Sawe akashinda marathon ya Valencia, ikawa sasa anatizama mbele tu, akijipangia mikakati yake.
2025 akawa bingwa wa marathon ya London akimaliza katika muda wa zaidi kidogo ya saa mbili.
Hiyo ilikuwa ni kama kupiga jaramba kwake na alivyorudi 2026 akamaliza mchezo, akiweka historia ya kuwa mwanariadha wa kwanza kumaliza marathon chini ya saa mbili.
Muda huo wa 1:59:30 pia ni rekodi ya dunia akiipiku rekodi iliyokuwepo ya mwaka 2023 kwa sekunde 65.
Miongoni mwa zawadi zingine Rais William Ruto wa Kenya amempa gari aina ya Mercedes Benz S-Class na kiasi cha fedha sawa na dola za Marekani zaidi ya 60,000
Mbali na kufurahia ushindi huo, na kupewa makaribisho muruwa nyumbani, Sabastian Sawe pia atapata zawadi za fedha kimataifa ikiwa ni pamoja na bonasi ya kuweka rekodi.
Je, mbio za marathon za wanaume sasa zimepata mfalme mpya?














