Tamasha la muziki la shule nchini Kenya lageuza mashindano kuwa sherehe za utamaduni
AFRIKA
4 dk kusoma
Tamasha la muziki la shule nchini Kenya lageuza mashindano kuwa sherehe za utamaduniWakati wanafunzi kutoka jamii mbalimbali wakishiriki katika kuimba nyimbo, na kupiga midundo kutumia ala za muziki za kimila, tamasha hilo linakuwa mahali pa kukutania utajiri wa utamaduni wa Kenya.
Kenya Music Festivals

Muziki unasikika katika shule na makumbi mbalimbali mjini Bungoma, magharibi mwa Kenya huku maelfu ya wanafunzi wakikusanyika kwa ajili ya Tamasha la Muziki la Shule na Vyuo nchini Kenya, mashindano ya kila mwaka yanayowakutanisha baadhi ya vijana wenye vipaji vya kipekee vya sanaa ya maonyesho nchini.

Kwa wanafunzi wanaoshiriki, kufika katika ngazi ya kitaifa ni mafanikio makubwa.

Stephen Asanga, mwanafunzi anayewakilisha Shule ya Upili ya Jamhuri jijini Nairobi, anaona kushiriki tamasha hili ni chanzo cha fahari, sio kwake yeye binafsi tu, bali pia kwa shule na familia yake.

"Kufika ngazi ya kitaifa ni mafanikio makubwa na heshima kwangu," Asanga anaiambia TRT Afrika. "Hii inanipa fursa ya kujiwakilisha mimi mwenyewe, shule yangu na familia yangu. Nitajitahidi kadiri niwezavyo kujifunza kutoka kwa wengine."

Maneno yake yanaakisi moja ya vipengele muhimu vinavyovutia katika tamasha hili. Ingawa wanafunzi hushindana ili kutambulika, pia wanapata fursa ya kukutana na kujifunza kutoka kwa wenzao wanaotoka sehemu mbalimbali za Kenya.

Na utofauti huo ndio unaoufanya muziki kuwa na mvuto wa kipekee.

Utamaduni na mila mbalimbali

Kwa wengine, tamasha hili hutoa fursa ya kusafiri na kuona tamaduni mbalimbali pamoja na kukutana na watu ambao wanatofautiana na mila zao.

"Naona tamaduni mbalimbali kupitia muziki kwa kusikiliza na kujifunza nyimbo, midundo, ala na mila zao," Alfa Wainaina anaambia TRT Afrika.

Anasema kuwa uzoefu huo umemfundisha sio tu kuhusu muziki, bali pia kuhusu heshima.

"Ninaheshimu tofauti za kitamaduni na kuthamini mchango wa kila utamaduni katika muziki," anasema.

Wakati wanafunzi kutoka jamii mbalimbali wakishiriki katika kuimba nyimbo, na kupiga midundo kutumia ala za muziki za kimila, tamasha hilo linakuwa mahali pa kukutania utajiri wa utamaduni wa Kenya.

Ulezi na mwongozo

"Kwa kufanya kazi pamoja, najifunza kutoka kwa wengine na wao pia hujifunza kutoka kwangu," anaongeza Wainaina. "Tunajenga urafiki na umoja. Muziki ni lugha ya kimataifa inayounganisha tamaduni mbalimbali."

Lakini nyuma ya maonyesho na mashindano hayo kuna hadithi nyingine — hadithi ya ulezi na mwongozo, pamoja na nafasi ya muziki katika kuunda maisha ya vijana.

Kwa Henry Wanjala, mkufunzi wa muziki katika Shule ya Upili ya Jamhuri, thamani ya muziki ilidhihirika wazi wakati wa kipindi kigumu ambapo shule kote nchini Kenya zilikuwa zikikabiliwa na machafuko, ikiwa ni pamoja na matukio ya kuchoma na uharibifu wa mali za shule.

Wakati huo, Wanjala anasema, waligundua kuwa kufundisha muziki pekee haikutosha.

"Muziki ulichukua asilimia 20. Asilimia 80 ya kazi tuliyokuwa tukifanya ilikuwa ni kutoa mwongozo na nasaha na malezi," Wanjala anaiambia TRT Afrika.

Nidhamu shuleni

Walimu walitumia shauku ya wanafunzi kwa muziki kama njia ya kuwafikia, kujenga uhusiano na wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali na kufanya mazoezi.

"Muziki ni sanaa wanayoipenda, na tuligundua kuwa hiyo ndio lugha inayowaunganisha," anasema Wanjala.

Kupitia uhusiano huo, na kwa kushirikiana na walimu wengine shuleni, waliweza kuzungumza na wanafunzi kuhusu nidhamu, kujituma, na matokeo yanayotokana na matendo yao.

Kwa Wanjala, kuwashirikisha wanafunzi katika jambo wanalolifurahia kuliwapa njia mbadala wakati ambapo wimbi la machafuko shuleni lingeweza kuwapotosha kwa urahisi.

"Tulibahatika kuwashirikisha katika jambo wanalolipenda ili wasiingizwe katika mienendo ya uharibifu wa shule iliokuwa ikiendelea," anasema.

Muziki unaweza kuwaunganisha watu

Sasa, tamasha la kitaifa linapoendelea mjini Bungoma, mafunzo hayo yanaonekana wazi katika maonyesho ya wanafunzi, kuanzia nidhamu inayohitajika wakati wa mazoezi, kujiamini wanapotoa burudani mbele ya hadhira, hadi utayari wao wa kujifunza kutoka kwa wengine.

Ingawa tamasha hilo linaweza kutoa washindi, athari zake ni kubwa zaidi kuliko vyeti na tuzo.

Kwa wanafunzi kama Asanga, ni fursa ya kuleta fahari kwa shule na familia zao.

Kwa Wainaina, ni fursa ya kufahamu tamaduni za watu wengine na kujenga urafiki.

Na kwa walimu kama Wanjala, ni uthibitisho kwamba muziki unaweza kuwa nyenzo madhubuti ya kutoa mwongozo, kuweka nidhamu, na kuhamasisha ushirikiano.

Hivyo, huko Bungoma, wasanii hao vijana wanashindana jukwaani, lakini pia wanapata mojawapo ya mafunzo ya kudumu zaidi ya tamasha hilo: kwamba muziki unaweza kuwaunganisha watu, licha ya tofauti zao za kiutamaduni, lugha na asili.

 

CHANZO:TRT Afrika