Kwa pamoja, madada hawa watatu kutoka Brazil, Levita mwenye umri wa miaka 109, Zoraide miaka 104, na Zulina miaka 103, kwa pamoja wamefikisha jumla ya miaka 316.
Ndugu hawa wameweka Rekodi ya Dunia ya Guinness kama madada walio na umri mkubwa zaidi.
Uhusiano wao umeendelea kuwa imara hata baada ya zaidi ya karne moja, ikiwa bado wanataniana, wanabishana mara kwa mara na kucheka pamoja.
Kwao, kuishi kwa afya hakukuwa mtindo wa maisha bali ndiyo yalikuwa maisha yenyewe.
Walikulia katika maisha tofauti kabisa na ya kizazi cha leo. Hakukuwa na simu, vyakula vya haraka, wala mitandao ya kijamii.
Walikuwa wanaogelea mtoni, wanavua samaki, wanatembea kila mahali na kula chakula cha asili.
Walikulia kijijini, katika maisha ya kawaida yaliyojengwa juu ya familia, chakula safi na kufanya kazi kwa bidii. Hakukuwa na jokofu wala vyakula vilivyosindikwa.
Levita, ambaye ndiye mkubwa, alichukua jukumu la kuwalea na kuwatunza wadogo zake wakati wazazi wao walipokuwa mashambani. Ingawa hakuolewa wala kupata watoto, alijitoa kuitumikia familia yake.
Alipenda kushona, kufuma na kusuka, vipaji vilivyompatia kipato na ambavyo ameendelea navyo hadi leo. Zoraide alianza kazi kama mwalimu wa shule ya msingi kabla ya kuwa muuguzi.
Akiwa pia mama wa watoto watano, anaamini msingi wa afya njema huanza tangu kuzaliwa, ikiwemo kula chakula cha asili kilichoandaliwa nyumbani. Kwa upande wake, Zulina alilea watoto sita na kuendeleza kipaji chake cha kushona na kudarizi.
Baada ya ndoa yake kuvunjika, alihamia Rio de Janeiro, Brazil ambako dada zake walimpokea na kuendelea kuwa pamoja.
Mpaka leo bado wanaishi karibu, wakisaidiana katika kila hatua ya maisha. Bila shaka, kila mmoja wetu anajiuliza siri ya maisha yao marefu.
Levita, Zoraide na Zulina wanatukumbusha kuwa pamoja na urithi wa kinasaba, maisha yenye lishe bora, kufanya shughuli za kila siku, kuwa na kusudi la kuishi na kudumisha upendo wa familia vinaweza kuwa sehemu ya safari ya kuishi maisha marefu na yenye afya.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha São Paulo nchini Brazil wanaichunguza vijinasaba vya DNA zao wakitumaini kubaini kwa nini wameendelea kuwa na afya njema ya mwili na akili licha ya kuvuka umri wa miaka 100.
Wanasayansi wanaamini huenda wakawa na vinasaba vinavyolinda mwili dhidi ya magonjwa na athari za uzee, jambo ambalo linaweza kusaidia kuboresha afya za vizazi vijavyo.
Simulizi ya madada watatu wenye umri zaidi ya miaka 100
Uhusiano wao umeendelea kuwa imara hata baada ya zaidi ya karne moja, ikiwa bado wanataniana, wanabishana mara kwa mara na kucheka pamoja.
Soma zaidi














