Sudan Kusini imejipatia Eneo lake la kwanza kabisa la Urithi wa Dunia.
Mandhari ya Boma–Badingilo iliorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Julai 26, 2026.
Hebu tuangalie fahari hii katika taifa changa zaidi barani Afrika.
Mandhari ya Boma–Badingilo, iliyoko kusini mashariki mwa Sudan Kusini, ni mojawapo ya mifumo muhimu zaidi ya ikolojia ya wanyamapori barani Afrika.
Inajumuisha Hifadhi za Taifa za Boma na Badingilo, na ni sehemu ya Great Nile Migration Landscape, eneo lenye ukubwa wa takribani hekta milioni 20 linalofika hadi Hifadhi ya Taifa ya Gambella nchini Ethiopia.
Eneo hili liko kati ya ardhi oevu ya Sudd na savana ya Mashariki mwa Sudan.
Lina nyasi pana, maeneo ya vinamasi, tambarare iliyojaa maji, misitu na savana zinazohifadhi viumbe hai wa kipekee.
Kila mwaka, takribani wanyamapori milioni sita wakiwemo swala ina huondoka katika eneo hili na kwenda kufuata mvua za msimu.
Huu ndio uhamaji mkubwa zaidi wa mamalia wa nchi kavu duniani, ukiwa mkubwa zaidi kuliko hata ule uhamaji maarufu wa Serengeti unaohusisha takribani wanyama milioni mbili.
Mfumo huu wa ikolojia pia ni makazi ya tembo, simba, chui, mbwa mwitu wa Afrika, duma, swala wa Nile pamoja na mamia ya aina za ndege.
Zaidi ya hayo, Boma–Badingilo linategemewa na jamii za asili kama Murle, Dinka, Nuer, Anyuak na Toposa, ambazo kwa karne nyingi zimekuwa zikijipatia kipato kupitia ufugaji, kilimo na uvuvi.
Kutambuliwa kwa Boma–Badingilo kama Eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO kumeipa Sudan Kusini hadhi mpya kimataifa.
Hatua hiyo imevutia wataalamu wa hifadhi, wapenda wanyamapori na watalii wa ikolojia kutoka duniani kote.
Pia imeimarisha taswira ya Sudan Kusini kama taifa lenye urithi wa kipekee wa asili, jambo linaloweza kuvutia uwekezaji katika miundombinu ya utalii na kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa.
Hata hivyo, utalii nchini humo bado haujaendelezwa ipasavyo kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2013, miaka miwili tu baada ya nchi hiyo kupata uhuru.
Mwaka 2022, Serikali ya Sudan Kusini ilisaini makubaliano ya miaka 10 na shirika la African Parks ili kusimamia na kuhifadhi mandhari hiyo pamoja na njia zake za uhamaji wa wanyamapori.
Licha ya umuhimu wake mkubwa wa kiikolojia, Boma–Badingilo bado inakabiliwa na changamoto kama ujangili, uharibifu wa makazi ya wanyamapori na athari za miongo kadhaa ya migogoro.
Baada ya kuorodheshwa na UNESCO, eneo hilo pia liliwekwa kwenye Orodha ya Maeneo ya Urithi wa Dunia Yaliyo Hatarini, hatua inayolenga kuhamasisha ufadhili wa kimataifa na kuongeza juhudi za uhifadhi wa urithi huu muhimu wa Afrika.

















