| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Nigeria: Wanawake 3 wafariki katika msongamano wakati wa kugawiwa Fedha
Maelfu ya watu walikusanyika Jumanne usiku katika makazi rasmi ya Gavana wa Jimbo la Niger, Mohammed Umaru Bago, ambapo kila mtu alitarajiwa kupokea naira 10,000, sawa na takribani Dola 7.50 za Marekani.
Nigeria: Wanawake 3 wafariki katika msongamano wakati wa kugawiwa Fedha
Mikanyagano wakati wa ugawaji wa fedha ni jambo la kawaida nchini Nigeria.

Wanawake watatu wamefariki dunia katika msongamano uliotokea wakati wa zoezi la kugawa fedha katika Jimbo la Niger, katikati mwa Nigeria, kwa mujibu wa madaktari waliozungumza na shirika la habari la AFP Jumatano.

Maelfu ya watu walikusanyika Jumanne usiku katika makazi rasmi ya Gavana wa Jimbo la Niger, Mohammed Umaru Bago, ambapo kila mtu alitarajiwa kupokea naira 10,000, sawa na takribani Dola 7.50 za Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya kiusalama iliyoandaliwa kwa ajili ya Umoja wa Mataifa na kuonekana na AFP, zoezi hilo la kugawa fedha lilipangwa, kwa sehemu, kuzuia maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufuatia kifo cha wachimbaji wadogo 37 waliokuwa wamekufa wakiwa chini ya ulinzi wa serikali takribani wiki mbili zilizopita.

Inadaiwa kuwa wachimbaji hao walifariki kwa kukosa hewa katika chumba kilichokuwa kimejaa watu na kisicho na mfumo mzuri wa uingizaji hewa. Vifo hivyo vilizua hasira na maandamano katika Jimbo la Niger.

Mhudumu wa afya katika Hospitali Kuu ya Minna, inayomilikiwa na serikali, alisema watu sita waliojeruhiwa pamoja na miili mitatu ililetwa hospitalini baada ya kutokea kwa msongamano huo.

“Miili yote ya waliofariki ilikuwa ya wanawake,” alisema mhudumu huyo wa afya, ambaye hakutaka kutajwa jina kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Hata hivyo, ripoti ya kiusalama ya Umoja wa Mataifa ilisema idadi ya waliofariki ni watu watano.

Polisi walisema bado walikuwa wakikusanya taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.

Yusuf Abubakar Bawa alisema binti yake mwenye umri wa miaka 15 alijeruhiwa katika msongamano huo na bado yuko katika hali ya kukosa fahamu.

Msongamano wa vifo Nigeria

Matukio ya watu kufariki kutokana na msongamano wakati wa ugawaji wa fedha au chakula yameripotiwa mara kadhaa nchini Nigeria. Baadhi ya zoezi hizo pia zinadaiwa kutokana na ushawishi wa kisiasa na rushwa ya kupigiwa kura kuelekea uchaguzi.

Mnamo Disemba 2024, watoto 35 walifariki dunia baada ya kutokea msongamano katika maonesho ya Krismasi mjini Ibadan, kusini-magharibi mwa Nigeria.

Mwezi Machi 2024, wanawake 17 walifariki katika msongamano uliotokea wakati wa ugawaji wa fedha katika Jimbo la Bauchi. Siku chache kabla ya tukio hilo, wanafunzi wawili walifariki katika msongamano mwingine uliotokea katika chuo kikuu katika Jimbo la Nasarawa.

Mnamo Julai 2021, zoezi la kugawa vocha za chakula kwa watu waliokuwa wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia za makundi ya kigaidi katika eneo la Monguno, kaskazini-mashariki mwa Nigeria, lilisababisha msongamano ulioua watu.

Aidha, mwezi Aprili 2020, zoezi jingine la kugawa misaada karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon lilisababisha msongamano na kuua takriban wanawake na watoto watano.

CHANZO:AFP