Kisa cha Kombe la Dunia kuibiwa mara mbili
Hadi kuibiwa kwake, kombe la Jules Rimet lilikuwa likimilikiwa na Brazil, baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo kulishinda kwa mara ya tatu mfululizo. / Others
Kisa cha Kombe la Dunia kuibiwa mara mbili
Hata hivyo, FIFA ilitambulisha Kombe jipya mwaka 1974, ambalo ndilo linatumika hadi sasa.

Wakati michuano ya Kombe la Dunia ikiendelea kurindima Marekani, Mexico na Canada, unafahamu kuwa kuliwahi kutokea wizi wa Kombe hilo katika matukio mawili ya kushangaza?

Likijulikana kama Jules Rimet, Kombe hilo la Dunia liliibiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1966, katika maonesho ya Stanley Gibbons huko Westminster jijini London, miezi minne kabla ya kutimua vumbi kwa michuano hiyo iliyofanyika nchini Uingereza.

Hali kubwa ya taharuki iliibuka ambapo kwa kuhofia kutopatikana kwa kombe hilo chama cha soka cha Uingereza (FA),  kwa siri kilipanga kutengeneza nakala nyingine lakini wiki moja baada ya msako mkubwa wa polisi kombe hilo lilikutwa na mbwa aitwaye Pickles.

Inadaiwa kuwa, wezi wa kombe hilo maarufu duniani walivunja kizuizi cha ulinzi na kuondoka na kombe hilo lililokuwa limenakshiwa kwa madini ya fedha na dhahabu.

Kombe hilo liliitwa Jules Rimet, kwa heshima ya rais wa tatu wa FIFA, Jules Ernest Séraphin Valentin Rimet.

Mbwa huyo alipewa hadhi ya shujaa wa taifa, baada ya kufanikisha upatikanaji wa Kombe la Dunia kwa mwaka huo.

Miaka 17 baadaye, kulitokea wizi mwingine wa Kombe la Dunia, huko Rio de Janeiro, Brazil.

Tukio hilo lilitokea Disemba 19, 1983, tuzo hiyo ikiibiwa kutoka kwenye kioo kisichoingiza risasi, ndani ya ofisi za Shirikisho la Soka la Brazil.

Tukio hilo linadaiwa kufanikishwa na mhalifu aliyejulikana kama Sérgio Pereira Ayres.

Tofauti na tukio la awali, kombe lililoibiwa nchini Brazil halikuwahi kupatikana, na inadaiwa kuwa liliyeyushwa na wahalifu hao, kwa nia ya kupata madini ya dhahabu kwa ajili ya kuuza.

Hadi kuibiwa kwake, kombe la Jules Rimet lilikuwa likimilikiwa na Brazil, baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo kulishinda kwa mara ya tatu mfululizo.

Hata hivyo, FIFA ilitambulisha Kombe jipya mwaka 1974, ambalo ndilo linatumika hadi sasa.

CHANZO:TRT Afrika Swahili