Wilaya ya Temeke inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waraibu wa dawa za kulevya mkoani Dar es Salaam, huku watu 2,500 waliokuwa wakitumia heroin wakipata huduma ya tiba mbadala ya methadone.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Temeke ndiyo wilaya yenye idadi kubwa zaidi ya watu walioathirika na uraibu wa dawa za kulevya, ikifuatiwa na Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kigamboni.
Akizungumza wakati wa tamasha la kupinga dawa za kulevya lililofanyika katika Viwanja vya Mwembe Yanga, Kamishna wa Divisheni ya Kinga, Tiba na Urejeshwaji, Dkt, Cassian Nyandindi amesema tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuwa kubwa katika Mkoa wa Dar es Salaam.
"Temeke inaongoza kwa kuwa na watu wengi walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Watu 2,500 waliokuwa wakitumia heroin wanatumia huduma ya methadone, jambo linaloonyesha ukubwa wa tatizo katika wilaya hii," alisema Dkt. Nyandindi.
Kulingana na Dkt. Nyandindi, mbali na huduma ya methadone, watu 16,000 wenye changamoto za afya ya akili zinazohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya wamepatiwa matibabu katika Wilaya ya Temeke tangu mwaka 2014.











