Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA Gianni Infantino anasema "hakuna shaka" Iran itashiriki Kombe la Dunia 2026 licha ya vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
"Iran itakuwepo bila shaka. Tunatarajia kufikia wakati huo hali itakuwa ya usalama, hilo litasaidia sana," Infantino alisema katika kituoc cha CNBC.
"Lakini Iran muhimu iwepo, wanawakilisha watu wao, wamefuzu, wachezaji wanataka kucheza," alisema kuhusu mechi zao zilizoratibiwa kuchezwa Marekani mwezi Juni.
Alisema kuwa "michezo haitakiwa kufungamanishwa na siasa."
"Kama hakuna mtu mwingine anayeamini katika kuunganisha watu, sisi tunalifanya hilo," aliendelea.
Matamshi yake yanakuja baada ya Mexico kuthibitisha kuwa FIFA imekataa ombi la Iran kuhamisha mechi zake zote kwa majirani wa Marekani wa kusini.
Wasiwasi wa kutoshiriki
Kumekuwa na wasiwasi wa Iran kushiriki kwenye mashindano hayo ya dunia kutokana na vita na Marekani na Israel vilivyoanza Februari 28.
Iran ilifuzu kwa Kombe la Dunia 2026 mwezi Machi 2025 baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Uzbekistan.
Kombe la Dunia, lina wenyeji wenza Marekani, Mexico na Canada, na linaanza Juni 11.
Hata hivyo, Iran imeratibiwa kucheza mechi zake zote za kundi G — dhidi ya Ubelgiji, Misri na New Zealand — nchini Marekani.
Kulingana na ratiba za mechi kwenye mtandao wa FIFA, Iran inatarajiwa kucheza dhidi ya New Zealand Juni 15 katika uwanja wa Los Angeles, Ubelgiji Juni 21 katika uwanja huohuo, na dhidi ya Misri Juni 26 katika uwanja wa Seattle.











