Mke wa Rais wa Zimbabwe: Auxillia Kutyauripo Mnangagwa
Auxillia Kutyauripo Mnangagwa ni mwanasiasa, mbunge wa zamani, na mhisani/ Picha: @ZimFirstLady
Mke wa Rais wa Zimbabwe: Auxillia Kutyauripo Mnangagwa
Kutyauripo amekuwa katika nafasi ya Mke wa Rais wa Zimbabwe tangu Novemba 24, 2017, baada ya mume wake Emmerson Mnangagwa kuapishwa rasmi kushika uongozi wa nchi hiyo.

Auxillia Kutyauripo Mnangagwa ni mwanasiasa, mbunge wa zamani, na mhisani.

Amekuwa katika nafasi ya Mke wa Rais wa Zimbabwe tangu Novemba 24, 2017, baada ya mume wake Emmerson Mnangagwa kuapishwa rasmi kushika uongozi wa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, aliwahi kuwa mbunge nchini Zimbabwe akiwakilisha jimbo la Chirumanzu–Zimbabwe kwa tiketi ya chama tawala cha ZANU–PF. Aliachia kiti chake cha ubunge baada ya kuwa Mke wa Rais mwaka 2017.

Alizaliwa Machi 21, 1963 katika Wilaya ya Mazowe, Mkoa wa Mashonaland Central.

Alihitimu mafunzo ya ukatibu kabla ya kuanza kazi katika Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Nguvu Kazi mwaka 1981.

Baadaye alifanya kazi katika sekta ya utalii na huduma nchini Zimbabwe na kisha kuendelea na masomo ya juu nchini Uswisi, ambapo alihitimu shahada ya Usimamizi wa Hoteli na Utalii mwaka 2001.

Pia alipata shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Midlands na aliendelea masomo ya Shahada ya Uzamivu.

Safari yake ya utumishi wa umma imechukua miongo kadhaa.

Alifanya kazi serikalini na baadaye kujiunga na uongozi wa ZANU–PF, akihudumu katika Kamati Kuu ya chama hicho kabla ya kuwa mbunge mwaka 2015.

Akiwa Mke wa Rais, Auxillia Mnangagwa amejikita katika masuala ya ustawi wa jamii, afya ya umma, uwezeshaji wa wanawake, haki za watoto, na maendeleo ya jamii.

Kupitia taasisi yake ya 'Angel of Hope Foundation,' amesimamia programu zinazounga mkono afya ya mama na mtoto, uelewa kuhusu saratani, tija katika kilimo, usalama wa chakula, mafunzo ya ufundi stadi, na misaada kwa jamii zilizo katika mazingira magumu.

Pia ameongoza kampeni za kuhamasisha upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti, lishe bora, na afya ya uzazi kote nchini Zimbabwe.

Nje ya Zimbabwe, ameshiriki katika mipango ya ngazi ya bara unaohusisha Wake wa Marais wa Afrika, akitetea uboreshaji wa huduma za afya, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, elimu, na maendeleo endelevu.

Pia ameshikilia nyadhifa za uongozi katika vyombo vya kibunge vya kikanda, ikiwemo Bunge la Pan-Afrika.

Auxillia Mnangagwa na Rais Emmerson Mnangagwa, wana watoto watatu.

Anajulikana sana nchini Zimbabwe kwa jina la heshima na upendo la "Amai" — likimaanisha "Mama" — jina linaloakisi msisitizo wake katika kuwafikia wananchi na kuendesha programu za kijamii.

CHANZO:TRT Swahili