Wake wa Marais : Tshepo Motsepe wa Afrika Kusini
Tshepo Motsepe ni mke wa rais wa Afrika Kusini / picha: Ikulu Afrika Kusini / Public domain
Wake wa Marais : Tshepo Motsepe wa Afrika Kusini
Dkt, Motsepe ni daktari wa binadamu akiwa na Shahada za Tiba, ya Upasuaji na Uzamili ya Afya

Tshepo Motsepe ni mke wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Aliolewa na Ramaphosa mwaka 1996, na kuwa mke wa Rais kuanzia 2018 wakati Cyril Ramaphosa kuwa rais wa Afrika Kusini.

Mzaliwa wa Soweto nchini Afrika Kusini Juni 1953 na kukulia katika vijiji vya Mathibestad karibu na Hammanskraal na katika jimbo la Kaskazini Magharibi.

Dkt. Motsepe ndiye mkubwa kati ya ndugu saba akiwemo Patrick Motsepe Rais wa Shirikisho la Soka Afrika.

Yeye ni daktari wa binadamu akiwa na Shahada ya Tiba na Shahada ya Upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal na Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma katika Afya ya Mtoto na Uzee kutoka Shule ya Harvard ya Afya ya Umma.

Pia ana Cheti cha Ujasiriamali wa Kijamii.

Dkt. Motsepe amefanya kazi hospitali za Afrika Kusini na Zimbabwe.

Pia alifanya kazi na Taasisi ya Afya ya Uzazi na utafiti wa Ukimwi ya Wits.

Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ithibati ya Idara ya Afya ya Gauteng.

Kwa sasa Dkt. Motsepe ni Mkuu wa wakfu wa Early Care Foundation, Shirika lisilo la kiserikali ambalo hutoa programu za usaidizi wa maendeleo ya watoto wachanga kwa vituo vya kufundishia majumbani katika jamii zisizojiweza.

Anahudumu kama kiongozi wa Shirika la Kiraia la Afrika Kusini la Afya ya Wanawake, Vijana na Watoto, Mpango wa Ufadhili wa Wanafunzi na mdhamini wa Chama cha Wauguzi cha Witwatersrand.

Katika kazi zake za kila siku, Dkt. Mosepe anasema anaongozwa na imani kwamba "maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni hitaji la lazima kwa jamii kuishi maisha yenye tija ''.

Ana watoto 4 pamoja na Rais Ramaphosa.

CHANZO:TRT Swahili