Umoja wa Wadau wa Kupata Taarifa nchini Tanzania (CoRI) umesema kuwa umepokea kwa masikitiko na wasiwasi mkubwa taarifa za uamuzi wa serikali ya kulifungia Gazeti la MwanaHalisi.
"Mamlaka za udhibiti zinapaswa kujiepusha na maamuzi yanayoweza kujenga hofu miongoni mwa waandishi na kufanya masuala ya umma kuwa mwiko kujadiliwa," imesema sehemu ya taarifa iliyotolewa na CoRI.
Wakati huo huo, CoRI pia imevitaka vyombo vya habari kuimarisha maadili, kuboresha mifumo ya habari za uchunguzi na kuzingatia uhakiki wa taarifa.
Hatua ya serikali ya kuifungia MwanaHalisi kwa miezi sita, inafuatia taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo yenye kichwa cha habari, "Nchimbi agoma kujiuzulu," ikidaiwa kukiuka masharti ya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017.
Gazeti la MwanaHalisi nchini Tanzania limekuwa na historia ndefu ya kufungia mara kwa mara, huku adhabu kali ikiwa ni ile ya Julai mwaka 2012, ambapo gazeti hilo lilifungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuandika habari zilizodaiwa kujenga hofu.
Hata hivyo, baadaye mwezi Machi 2021, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitengua adhabu hiyo.












