Mahakama Kuu ya Tanzania imemkuta na kesi ya kujibu, Mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu katika kesi yake ya uhaini.
Uamuzi huo umetolewa Ijumaa ya Agosti 21, 2026 na kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, wakiongozwa na Dunstan Ndunguru.
Uamuzi huo, unakuja baada ya Mahakama hiyo, kusikiliza hoja na ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili.
Mahakama imeeleza kuwa, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa pamoja na maudhui yaliyomo kwenye hati ya mashtaka, imejiridhisha kuwa kuna msingi wa kisheria wa mtuhumiwa kuendelea kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Kwa sasa, mwanasiasa huyo anatarajiwa kuanza hatua ya utetezi ambapo ametaja mashahidi 11 watakaotoa ushahidi kwa upande wake.

















