Serikali imezindua upya reli ya zamani ya Thomson Falls, kuunganisha tena Mkoa wa Kati ya kenya, Ol Kalou na Nyahururu kwa mtandao wa kitaifa wa reli kupitia njia iliyofufuliwa ya Gilgil–Nyahururu.
Huduma za abiria na mizigo zinarejea katika njia hiyo ambayo ilikuwa imesimama tangu mwaka wa 1980.
Hapo awali reli hiyo ilijengwa mwaka wa 1929 wakati wa ukoloni, hasa kwa ajili ya kuhudumia mashamba ya wazungu wakoloni ya maeneo yanayoitwa Highlands na kusafirisha mazao ya kilimo, mbao na mifugo kutoka mikoa yenye rutuba ya Nyandarua na Laikipia hadi kwenye masoko makubwa.
Kuwasili kwa reli hiyo kulisaidia kubadilisha taswira ya mji ambao wakati huo uliitwa kwa jina Thompson falls, kwa ajili ya maporomoko maarufu ya maji katika eneo hilo, na baadaye kulibadilishwa jina kuwa Nyahururu na kuwa kituo kikuu cha kibiashara.
Reli iliharibiwa
Njia hiyo pole pole iliacha kutumika mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980 kufuatia kuporomoka kwa mfumo wa Reli wa Afrika Mashariki, kupungua kwa idadi ya abiria na mizigo, kupanda kwa gharama za usimamizi na kuongezeka kwa ushindani kutokana na usafiri wa barabarani.
Kwa miaka mingi, miundombinu ya reli hiyo iliharibiwa, kuibiwa na kuachwa kutelekezwa.
Leo, watu wengi wanaosafiri kati ya Nairobi, Gilgil, Ol Kalou na Nyahururu wanategemea usafiri wa barabara, ikiwa ni pamoja na mabasi, matatu, magari binafsi na lori ya mizigo yanayotumia mtandao wa barabara kuu ya Nakuru-Nyahururu.
Reli iliyofufuliwa inatoa njia mbadala inayoweza kuwa nafuu kwa usafirishaji wa shehena nyingi kama vile mbolea na mazao ya mashambani huku ikipunguza shinikizo barabarani.
Reli zingine zilizosahaulika
Shirika la Reli la Kenya linasema huduma ya kwanza ya uchukuzi iliyofufuliwa tayari imefikisha karibu tani 400 za mbolea Ol Kalou na Nyahururu, huku huduma mpya ya abiria ikitarajiwa kuunganisha eneo hilo na Nairobi.
Na hii sio reli pekee ya wakati wa ukoloni ambayo Kenya imejaribu kufufua.
Njia nyengine za reli za kihistoria ambazo ziliachwa au kutelekezwa ni pamoja na:
* Reli ya Nairobi–Nanyuki, iliyojengwa miaka ya 1920 na kufufuliwa mwaka wa 2020.
* Reli ya Magadi, iliyojengwa awali mwaka wa 1915.
* Reli ya Kitale, iliyofunguliwa mwaka wa 1926.
* Reli ya Solai.
* Reli inayounganisha Eldoret hadi mpaka na Uganda.
* Reli ya Kisumu–Butere.
Kwa Wakenya wengi, kufufuliwa kwa Reli ya Thomson Falls ni zaidi ya kuimarishwa kwa usafiri, ni ufufuo wa kipande cha historia ya reli ambayo ilisaidia kujenga mkoa wa kati ya Kenya karibu karne moja iliyopita.



.jpg?width=720&format=webp&quality=80)


.jpg?width=128&format=webp&quality=80)












