Serikali ya Tanzania imeifunga rasmi kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Kambi hiyo, ilikuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi, kwa muda mrefu.
Maamuzi hayo, yanafuatia hatua ya wakimbizi zaidi ya 160,000 waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi hiyo kurudishwa nchini mwao.
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Patrobas Katambi, uwepo wa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi ya Nduta, ni ishara ya wazi ya kuvurugika amani nchini Burundi.
Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Zulqarnain Hussain, ameishukuru Tanzania kwa moyo wa ukarimu wa kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi hao, ambao waliishi kwa amani muda wote.
Tanzania ilianza kuhifadhi wakimbizi wa Burundi katika kambi hiyo mwaka 2016, wakipokea wakimbizi 125,000 na hadi kambi inafungwa jumla ya wakimbizi zaidi ya 166,330 walikuwa wamerejeshwa Burundi, baada ya hali ya usalama nchini mwao kuimarika.









