Wananchi wa Ethiopia wamejitokeza kwa wingi kupiga kura Jumatatu, huku chama tawala cha Prosperity Party (PP) kinachoongzwa na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed, kikitarajiwa kupata ushindi mkubwa, kwa mujibu wa wachambuzi.
Abiy ameiongoza nchi hiyo ya Pembe ya Afrika yenye watu milioni 130 tangu mwaka 2018. Mwaka 2019, alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na juhudi zake za kurejesha uhusiano mzuri na nchi jirani ya Eritrea.
Waandishi wa habari wa AFP walishuhudia foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura jijini Addis Ababa, Ethiopia. Baadhi ya wapiga kura wamekuja na viti ili kupunguza usumbufu wa kusubiri kwa muda mrefu.
"Ni wakati muhimu wa kuamua hatima ya nchi yetu," alisema Binyam Gideyelem, mwenye umri wa miaka 38, mfanyakazi wa mawasiliano ya simu aliyekuwa akipiga kura kwa mara ya kwanza katika kituo kilicho karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa.
"Ninataka kutumia haki yangu kama raia binafsi," aliongeza Seife Desta, mwenye umri wa miaka 77.
Upinzani uliogawanyika
Uchaguzi huu "una uwezekano mkubwa wa kuwa miongoni mwa chaguzi zisizo na ushindani mkubwa zaidi kati ya chaguzi saba za kitaifa zilizofanyika tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanzishwa mwaka 1991," kwa mujibu wa Ahmed Soliman na Abel Abate Demissie katika makala walioandika kwa taasisi ya utafiti ya Chatham House wiki iliyopita.
Katika uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2021, chama cha PP cha Abiy kilishinda asilimia 96 ya viti vya bunge.
Vyama vya upinzani vinaingia kwenye uchaguzi huu vikiwa na rasilimali chache za kifedha na vimegawanyika katika zaidi ya vyama 40. Katika majimbo mengi ya uchaguzi, chama tawala kinagombea bila mpinzani.
Chatham House ilibainisha kuwa: "Wapinzani wengi wa chama tawala cha PP hawatashiriki uchaguzi. Baadhi wako uhamishoni, baadhi wamepigwa marufuku, wengine wamefungwa gerezani, na wengi hawaoni sababu ya kuacha mapambano yao ya silaha dhidi ya serikali."
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12:00 asubuhi kwa saa za eneo hilo (0300 GMT) na vinatarajiwa kufungwa saa 12:00 jioni. Zaidi ya watu milioni 50 wamesajili kupiga kura katika vituo 48,000 vya kupigia kura vilivyoko kote nchini.
Matokeo yanatarajiwa kutangazwa takriban siku 10 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.
Migogoro ya kivita
Hakuna uchaguzi unaofanyika katika eneo la kaskazini la Tigray kutokana na mvutano unaoendelea kati ya mamlaka za kikanda na serikali kuu. Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2020 na kuendelea hadi 2022.
Licha ya changamoto hizo, uchumi wa Ethiopia unaendelea kukua kwa kasi kubwa na ni miongoni mwa uchumi unaokua kwa haraka zaidi duniani. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linatarajia ukuaji wa zaidi ya asilimia 9 mwaka huu.
Ukuaji huo unatokana kwa kiasi kikubwa na uwekezaji katika miundombinu na viwanda uliofanywa na serikali zilizopita, ingawa mageuzi ya kiuchumi ya kufungua soko yaliyofanywa chini ya uongozi wa Abiy yameongeza mauzo ya nje licha ya kuleta changamoto za muda mfupi kwa watumiaji wa Ethiopia.
Migogoro katika majimbo mawili yenye idadi kubwa ya watu, Oromia na Amhara, bado haionyeshi dalili za kupungua.
Katika Amhara, yenye wakazi takriban milioni 20, wanamgambo wa kitaifa wa Fano wametishia kuvuruga mchakato wa uchaguzi. Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefuta upigaji kura katika majimbo 8 pekee kati ya majimbo 137 ya uchaguzi katika eneo hilo.
Tume hiyo inasisitiza kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kote katika eneo kubwa la Oromia, linalochukua karibu theluthi moja ya eneo la nchi, ambako waasi wa Jeshi la Ukombozi la Oromia (OLA) wamekuwa wakifanya shughuli zao tangu mwaka 2018.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, wenye makao makuu Addis Ababa, pamoja na jumuiya ya kikanda ya IGAD, wanafuatilia uchaguzi huo wa Jumatatu.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Ethiopia ilikataa pendekezo la EU la kutuma waangalizi wa uchaguzi.




















