Mahakama kuu nchini Kenya imeamuru kusimamishwa kwa muda kwa mipango ya Marekani kuanzisha kituo cha karantini cha Ebola nchini humo.
Jaji wa Mahakama Kuu Patricia Nyaundi alisema katika maagizo yake Alhamisi jioni kwamba Kenya pia hairuhusiwi kuruhusu mtu yeyote aliyeambukizwa au kushukiwa kuambukizwa Ebola chini ya makubaliano yaliyopangwa na Marekani, hadi kesi ya kupinga mpango huo isikizwe na kuamuliwa.
Marekani ilikuwa imeripotiwa kufikia makubaliano na Kenya kuanzisha kituo cha karantini na matibabu ya Ebola chenye vitanda 50 katika kambi ya jeshi la anga huko Laikipia, mahsusi kwa Wamarekani waliokabiliwa na mlipuko wa Ebola unaoendelea nchini DR Congo na Uganda.
Kituo hicho kilitarajiwa kuwa na wafanyikazi wa afya ya umma wa Marekani na kufadhiliwa na Idara za Ulinzi, ya Marekani.
Lakini mpango huo ulizua hasira nchini Kenya.
Kundi la kutetea haki za binadamu, Katiba Institute pamoja na Chama cha Wanasheria wa Kenya walikimbilia mahakamani wakisema kuwa mpango huo ulikuwa wa siri, kinyume cha katiba na hatari.
Ombi hilo linadai Wakenya hawakushauriwa, Bunge halikuwahi kuidhinisha mpango huo na hakukuwa na tathmini ya wazi ya mazingira au afya ya umma.
Walalamishi hao pia walidai kuwa Kenya haina maabara za kiwango cha juu zaidi cha Usalama cha ngazi ya 4 ambazo kawaida huhusishwa na kushughulikia magonjwa hatari kama Ebola.
Sasa Mahakama Kuu imetoa maagizo ya kuzuia serikali kwa muda kuanzisha, kuidhinisha au kuendesha karantini yoyote ya Ebola, kutengwa au kituo cha matibabu kinachohusishwa na Marekani au serikali yoyote ya kigeni.
Wakosoaji wanasema mpango huo ulihatarisha kugeuza Kenya kuwa kile wanachokiita "kituo cha karantini cha nje" kwa nchi za kigeni. Wanaounga mkono hata hivyo wanahoji kuwa kituo hicho kinaweza kuimarisha utayari wa kudhibiti magonjwa nchini Kenya na kuleta ufadhili wa kimataifa na vifaa.
















