Kutoka kuwa mchunga ngamia hadi mpiga picha: Safari ya Ahmed Luzako
Ahmed Luzako ametimiza ndoto yake ya kuwa mpiga picha hodari nchini Somalia. / Wengine
Kutoka kuwa mchunga ngamia hadi mpiga picha: Safari ya Ahmed Luzako
Akiwa na tabasamu na kuonekana mtulivu, ukarimu ukiwa sehemu ya maisha yake, Ahmed Luzako ana haiba ya kijana aliyekulia mjini — ila chimbuko la maisha yake ni maeneo ya vijijini.

Na Mohammed Hirmoge

Ahmed Luzako anaonesha matumaini akiwa amevalia mavazi yake nadhifu. Yeye ni mpiga picha. Na ni hivi karibuni tu ambapo alipata shahada ya Sayansi ya Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Somalia.

Lakini pamoja na hayo na muonekano wake kuna simulizi ya vumbi, mwendo mrefu, na imani thabiti. 2020, Luzako alikuwa bado katika shule moja kijijini kwao.

Akienda shule mchana na jioni majukumu ya kuchunga ngamia yakimsubiri. Kabla ya kuingia Chuo Kikuu na kujishughulisha na utaalamu wa upigaji picha, darasa lake lilikuwa katika eneo la wazi, na majukumu yake ya kila siku ilikuwa mazingira ya kupambana na hali ngumu.

Jina lake ni Ahmed Mohamed Dahir. Alizaliwa 2002 katika kijiji cha Hiiraan, karibu na mpaka wa Somalia na Ethiopia. Ni mmoja kati ya watoto kumi, aliyelelewa na wazazi wake ambao bado wako pamoja, katika misingi ya ustahmilivu.

Wao ni miongoni mwa jamii ya kuhama hama. Na popote wanapofahamu kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa mvua na malisho ya mifugo wanaweka makazi hapo.

Hofu kubwa ilikuwa ni kiangazi.  Mvua ilikuwa matumaini kwao. Na wale tu waliokuwa na ustahmilivu, ndiyo waliofanikiwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.

2009, Ahmed alianza elimu yake ya msingi, akijikita katika mafunzo ya Qur’an na masomo mengine katika kijiji kidogo cha Gerijir, ambacho sasa hivi ni wilaya. Alikuwa na shughuli nyingi za kila siku, asubuhi akiingia darasani, mchana akichunga mifugo. Si kazi rahisi, lakini ilibidi aifanye.

Mwaka 2017, alimaliza shule ya msingi. Akawa na lengo la kuendeleza masomo yake, akaelekea eneo la Guriel kuendelea na masomo yake ya shule ya upili. Hata wakati huo, hakusahau maisha yake ya ufugaji. Siku za Alhamisi na Ijumaa alirudi kuangalia mifugo yake. Elimu haikuchukua nafasi ya majukumu yake; aliendeleza yote kwa pamoja.

Kufikia 2020, wakati vijana wengi kutoka kijiji chake wakisafiri kuelekea mjini Mogadishu kutembelea jamaa zao au pengine kutizama mandhari ya mji kuu, Luzako alikuwa na malengo tofauti. Alifahamu kuwa ametoka kwenye familia ya wafugaji ambayo maisha yao ni ishara ya ustahmilivu. Nia yake  haikuwa kukimbia maisha hayo, bali alijiwekea malengo mahsusi.

Akiwa mjini Mogadishu, alimaliza masomo yake ya shule ya sekondari 2021. Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Taifa cha Somalia kujifunza Sayansi ya Kompyuta.

Kuingia Chuo Kikuu kulibadilisha mtazamo wake. Pamoja na masomo yake, alipata fursa ya kutambua kitu kingine kinachomfurahisha, kutumia kamera na kupiga picha.

Alianza kujifunza na kuimarika katika tasnia hiyo. Kile kilichoanza kama jambo la kujifurahisha ikawa ndiyo taaluma yake. Aliimarisha uhodari wake na kufika viwango vya ubora zaidi.

Kwa umahiri huo alipata fursa ya kufanya kazi na mashirika ya kimataifa, na kufanikiwa kutembelea karibu kila kanda ya nchi ya Somalia.

2026, alikamilisha masomo yake ya shahada Chuo Kikuu.

Kutoka kuchunga ngamia hadi kuhariri picha, kutoka kwenye maeneo kame hadi kupata shahada ya Chuo Kikuu, safari ya Ahmed siyo tu ya kuvuka mabonde na milima, ni safari inayodhihirisha uwezekano wa kubadilisha muonekano.

Na bado akiwa na kamera yake, ndiyo mwanzo mkoko unaalika maua kwa Ahmed Luzako.

CHANZO:TRT Afrika Swahili