Sarah Mullally anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Kanisa la Uingereza ndani ya miaka 1,400, baada ya kusimikwa kama askofu wa jimbo la Canterbury, siku ya Jumatano.
Sherehe hizo za kumsimika uaskofu, zilihudhuriwa na wageni wapatao 2,000, ikiwemo familia ya kifalme ya Uingereza.
"SikuwaHI kufikiria kuifikia siku hii, hususani wito huu niliyoitiwa,” alisema Mullally wakati akitoa mahubiri yake kwa mara ya kwanza.
Oktoba mwaka jana, kanisa la Anglican la nchini Uingereza, lilimtangaza Mullaly, mwenye umri wa miaka 64, kama askofu ajaye wa jimbo la Canterbury, akichukua nafasi ya Justin Welby.
Welby alijiuzulu mwezi Novemba 2024, kufuatia madai ya kutokuchukua hatua zozote kuhusiana na taarifa alizokuwa nazo kuhusu namna ya kuzuia manyanyaso ya watoto.
Kanisa la Uingereza liliruhusu kuwasimika wanawake kama maaskofu mwezi Julai mwaka 2014, huku sheria hiyo ikipitishwa na kuanza kutumika mwaka huo huo.
Hata hivyo, mijadala kuhusu jinsi na jinsia ilizidi kutawala, baada ya Mullally kuchaguliwa kama askofu wa jimbo la London mwaka 2017, na kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.














