Muungano wa kimataifa wa ‘Zero Waste’ wapata uungwaji mkono wa Kimataifa katika mkutano wa COP31
UTURUKI
6 dk kusoma
Muungano wa kimataifa wa ‘Zero Waste’ wapata uungwaji mkono wa Kimataifa katika mkutano wa COP31Wake wa viongozi wa nchi mbalimbali pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa wamepongeza uongozi wa Emine Erdogan katika kuendeleza mpango wa kutokuwepo taka, wakitaka ushirikiano wa kimataifa uimarishwe zaidi kupitia ufadhili.
Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, mwenyeji wa chakula cha mchana kwa ajili ya wake wa viongozi wa nchi mbalimbali mjini Antalya. / / َAA

Wake wa viongozi wa nchi mbalimbali na maafisa waandamizi wa kimataifa wameeleza kuunga mkono kuanzishwa kwa Muungano wa Kimataifa wa Kutokuwepo Taka (Global Zero Waste Alliance), wakieleza kuwa mpango huo unaoongozwa na Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, una uwezo wa kuwa vuguvugu la kimataifa litakalosababisha kuchukuliwa kwa hatua za pamoja katika kukabiliana na tatizo la taka linalozidi kuongezeka.

Wakizungumza katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wake wa Viongozi wa Nchi, uliofanyika siku ya Ijumaa pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) mjini Antalya, washiriki waliupongeza muungano huo na kutoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano, upatikanaji wa ufadhili endelevu na ushiriki mpana zaidi wa wananchi ili kufanikisha malengo yake.

Ziroat Mirziyoyeva, mke wa Rais wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev, aliupongeza uongozi wa Erdogan, akisema kuwa mpango wa kutokuwepo taka umeendelea kukua na kuwa vuguvugu la kimataifa.

"Mpango wa kutokuwepo taka ulioanzishwa chini ya uongozi wako leo umegeuka kuwa vuguvugu la kimataifa," alisema, huku akieleza kuwa Uzbekistan inatoa uungwaji mkono wake kamili kwa kuanzishwa kwa Muungano wa Kimataifa wa Kutokuwepo Taka.

Mirziyoyeva alisema kuwa msingi wa mpango huo ni kuthamini rasilimali za asili, kuzuia uzalishaji wa taka na kutimiza wajibu kwa vizazi vijavyo.

Alionya kuwa ongezeko la idadi ya watu na matumizi ya bidhaa na huduma vinachangia kuongezeka kwa taka, akiashiria makadirio ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) yanayoonesha kuwa taka zinaweza kufikia tani bilioni 3.8 kwa mwaka ifikapo 2050.

Pia alieleza wasiwasi wake kuhusu makadirio yanayoonesha kuwa takribani tani bilioni moja za chakula hutupwa duniani kila mwaka.

Akibainisha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuwa kali katika Asia ya Kati, Mirziyoyeva alisema kuwa utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi vimekuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu vya sera za kitaifa za Uzbekistan.

‘Inatia moyo kwa namna ya pekee’

Dkt. Zubaida Rahman, mke wa Waziri Mkuu wa Bangladesh, Tarique Rahman, pia aliupongeza muungano huo, akielezea uongozi wa Emine Erdogan katika kuendeleza ajenda ya kutokuwepo taka kuwa "wa kutia moyo kwa namna ya pekee".

Alisema mpango huo unaendana na dira ya Bangladesh ya kuwa na mazingira safi zaidi, jamii zenye afya bora na mustakabali endelevu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kufikia lengo la kutokuwepo taka kunahitaji ushirikiano wa kimataifa, ukiwemo upatikanaji wa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa gharama nafuu, utumiaji wa teknolojia na msaada wa kujenga uwezo.

Dkt. Zubeida pia alitoa wito wa kuongeza ushiriki wa vijana, akisema kuwa vijana hawapaswi kuonekana tu kama viongozi wa kesho, bali pia washirikishwe katika kutafuta suluhisho za changamoto zilizopo leo.

Anaclaudia Rossbach, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Makazi ya Watu (UN-Habitat), aliipongeza hatua ya mpango huo kukua na kuwa vuguvugu la kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuyasaidia mamlaka za serikali za mitaa kuendeleza miji safi na endelevu zaidi.

Alisema UN-Habitat inashirikiana na mamlaka za serikali za mitaa kutathmini mifumo ya usimamizi wa taka na kupanua huduma zinazohusiana na eneo hilo. Pia alisisitiza nafasi muhimu ya wanawake katika kusababisha mabadiliko ndani ya jamii na kaya.

Anaclaudia alisema muungano huo mpya unaweza kusaidia kuwaunganisha viongozi wa kisiasa na wataalamu wa kiufundi, akiongeza kuwa UN-Habitat iko tayari kuchangia katika juhudi zake.

Ajenda ya kimataifa

Alexander De Croo, Msimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), pia aliukaribisha mpango huo na kumshukuru Emine Erdogan kwa kuiweka ajenda ya kutokuwepo taka na hatua za kulinda mazingira katika mjadala wa kimataifa.

Alibainisha uhusiano uliopo kati ya taka na uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani, hususan gesi ya ‘methane’, akisisitiza kuwa kupunguza kutupwa kwa chakula ni hatua muhimu katika kupunguza uzalishaji huo.

De Croo alisema kuwa uchumi unaozingatia matumizi endelevu ya raslimali unaweza kutoa mchango mkubwa katika juhudi za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani.

Janja Lula da Silva, mke wa Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, alieleza changamoto zinazoikabili nchi yake, ambayo huzalisha takribani tani milioni 90 za taka kila mwaka.

Alisema kuwa chini ya asilimia 4 ya taka hizo huchakatwa au kutumika tena, licha ya Brazil kuwa na sera ya kitaifa ya taka iliyoanzishwa mwaka 2010, inayoweka kipaumbele katika kupunguza uzalishaji wa taka, na uchakataji wa taka.

Jannja alisema sera hiyo pia iliweka mfumo wa kugawana majukumu katika mnyororo mzima wa uzalishaji na matumizi ya bidhaa, kwa kuwataka wadau kuweka mifumo ya uchakataji baada ya matumizi, zikiwemo vifaa vya kielektroniki na dawa.

Alionya kuwa mbinu zisizofaa za uchakataji zinaiingizia Brazil hasara ya takribani bilioni 120 kila mwaka, akionesha kuwa usimamizi duni wa taka una madhara ya kiuchumi sawa na yale ya kimazingira.

Hatua za pamoja

Sajidha Mohamed, Mke wa Rais wa Maldives, alielezea uendelevu wa mazingira kuwa suala linalohusu moja kwa moja uhai na mustakabali wa nchi yake, ambayo mifumo yake ya ikolojia iliyo katika hali tete inakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka vinavyotokana na taka, hususan uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na plastiki.

Alionya kuwa taka zinazoelea baharini zinaharibu miamba ya matumbawe na kuvuruga minyororo ya chakula, huku akimpongeza Emine Erdogan kwa uongozi wake katika kuendeleza vuguvugu la kimataifa la kukabiliana na taka.

Sajidha alisema kuwa Muungano wa Kimataifa wa Kutokuwepo Taka unatoa fursa muhimu ya kubadilisha malengo yanayofanana miongoni mwa nchi kuwa hatua za pamoja, akiongeza kuwa anaunga mkono kwa dhati dira na malengo yake.

Ancelly Simina, mke wa Rais wa Micronesia, Wesley W. Simina, alisema kuwa usimamizi madhubuti wa taka ni muhimu katika kulinda mazingira, kuhifadhi afya ya umma na kuhakikisha mustakabali endelevu kwa jamii zinazoishi visiwani.

Alieleza kuwa nchi yake inaweka mkazo katika utungaji wa sera, uhamasishaji wa umma, usimamizi wa maeneo ya kutupia taka, utupaji taka na uchakataji. Alisisitiza kuwa kuelekea katika mfumo wa kutokuwepo taka kunahitaji dhamira ya kudumu na ushiriki hai wa jamii nzima.

Zeinab Suleman, mkwe wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, naye alieleza kuwa Pakistan inaunga mkono muungano huo, akibainisha uhusiano uliopo kati ya uwajibikaji wa kimazingira, afya ya umma, fursa za kiuchumi na utu wa binadamu.

Alitoa wito kwa shule na kaya kuzingatia mbinu bora za ununuzi na uhifadhi wa chakula ili kuzuia kutupwa kwa chakula, sambamba na kutenganisha taka, uchakataji wa taka.

Zeinab pia alisisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii za maeneo husika katika mipango ya utunzaji wa mazingira na kuhakikisha mazingira salama zaidi ya kazi kwa wafanyakazi. Alisema Pakistan iko tayari kushirikiana na nchi nyingine kwa kubadilishana uzoefu na matokeo ya vitendo.

Alipendekeza kuwa nchi zitakazoshiriki katika mpango huo ziweze kuwasilisha maendeleo na matokeo ya utekelezaji wa juhudi zao katika COP32.

Wakati huohuo, Gueta Selemane Chapo, mke wa Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, alisema kuwa usawa wa tabianchi hauwezi kufikiwa wakati mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa huku chakula, maji na rasilimali za asili zikiendelea kutumiwa vibaya.

Alieleza kuwa kulinda rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo, wakiwemo wale ambao bado hawajazaliwa, ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili kizazi cha sasa.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na maoni Nilden Bektaş Erhurman, mke wa Rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini, Tufan Erhurman, pamoja na Francine Ntakarutimana wa Burundi, miongoni mwa washiriki wengine.

Uzinduzi wa Muungano wa Kimataifa wa Kutokuwepo Taka katika COP31 unaashiria hatua nyingine katika juhudi za kupanua ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza uzalishaji wa taka, kuimarisha uchakataji wa taka na kuendeleza matumizi endelevu ya rasilimali.

CHANZO:TRT World