Mamilioni ya watu wanaweza kukumbwa na njaa kali ikiwa mbolea haitaruhusiwa kupita haraka katika Mlango-Bahari wa Hormuz, UN imeonya.
“Tuna wiki chache zijazo kuzuia kile kinachoweza kuwa mgogoro mkubwa wa kibinadamu,” alisema Jorge Moreira da Silva, mkurugenzi mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS) na kiongozi wa kikosi kazi hicho, katika mahojiano jijini Paris siku ya Jumatatu.
“Tunaweza kushuhudia mgogoro utakaosukuma watu milioni 45 zaidi kwenye njaa na ukosefu mkubwa wa chakula.”
Iran imekuwa ikidhibiti njia hiyo muhimu ya bahari kwa miezi kadhaa kama hatua ya kulipiza kisasi kutokana na vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel tarehe 28 Februari.
Njia hiyo hupitisha takribani theluthi moja ya mbolea ya dunia, na usumbufu wake umeathiri biashara muhimu kwa wakulima duniani wakati nchi nyingi zikiwa katika msimu muhimu wa kupanda mazao.
Katibu Mkuu wa UN alianzisha kikosi kazi hicho mwezi Machi ili kuandaa mfumo utakaowezesha mbolea na malighafi zake kama amonia, salfa na urea kupita salama kwenye mlango huo wa bahari.
Afrika na Asia kuathirika zaidi
Kwa wiki kadhaa, Moreira da Silva amekuwa akijaribu kushawishi pande zinazohasimiana kuruhusu hata meli chache zipite, na pia amekutana na zaidi ya nchi 100 kupata uungwaji mkono ndani ya Umoja wa Mataifa.
Amesema idadi inayoongezeka ya nchi zinaunga mkono mpango huo, lakini Marekani, Iran, na nchi za Ghuba—ambazo ni wazalishaji wakuu wa mbolea—bado hazijaunga mkono kikamilifu.
Ingawa matumaini ya mwisho ni kufikia makubaliano ya amani ya kudumu na uhuru wa usafirishaji wa bidhaa zote kupitia njia hiyo, alisema “msimu wa kupanda hauwezi kusubiri,” kwani baadhi ya msimu huo katika nchi za Afrika utaisha ndani ya wiki chache.
Ulimwengu umezingatia zaidi athari za kiuchumi za usumbufu wa mafuta na gesi, lakini UN imeendelea kuonya kuhusu hatari ya mgogoro huu kwa usalama wa chakula duniani, ambapo Afrika na Asia zinatarajiwa kuathirika zaidi.
Ongezeko kubwa la gharama za mbolea
Moreira da Silva alisema UN inaweza kuanzisha mfumo wa dharura ndani ya siku saba, lakini hata kama njia hiyo ingefunguliwa sasa, itachukua miezi mitatu hadi minne kurejea hali ya kawaida.
“Ni suala la muda tu. Kama hatutazuia chanzo cha mgogoro huu mapema, tutalazimika kushughulikia matokeo yake kupitia misaada ya kibinadamu.”
Ingawa bei za chakula bado hazijapanda kwa kiwango kikubwa, alisema gharama za mbolea zimepanda sana, jambo ambalo wataalamu wanasema linaweza kupunguza uzalishaji wa kilimo na kusababisha kupanda kwa bei za chakula duniani.
Alisema kama meli tano kwa siku za mbolea na malighafi zingepita kupitia mlango huo, ingeweza kuzuia mgogoro kwa wakulima.
Kilicho muhimu zaidi, alisema, ni “uwepo wa nia ya kisiasa.”
“Hatuwezi kuahirisha mambo ambayo yanaweza kufanya na ambayo ni ya muhimu—yaani kuruhusu mbolea ipite na hivyo kupunguza hatari ya uhaba mkubwa wa chakula duniani.”
















