Mahakama nchini Burkina Faso, imemhukumu waziri wa zamani wa Masuala ya Kiutu, Laure Zonga, kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya wizi wa fedha za umma, kujitajirisha kwa njia haramu pamoja na utakatishaji wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa za Mahakama, Zonga alihusishwa na ubadhirifu wa kiasi cha Dola 61,400, fedha zinazodaiwa kupatikana au kutumika kinyume cha sheria wakati akiwa madarakani, jambo lililosababisha uchunguzi na baadaye kufikishwa Mahakamani.
Hukumu hiyo imekuja katika kipindi ambacho utawala wa nchi hiyo, unaoongozwa na Ibrahim Traore, ukiweka mkazo mkubwa katika kusafisha mifumo ya utawala na kuwajibisha viongozi wanaohusika na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mbali na mapambano dhidi ya ufisadi, Rais Traore, pia ameainisha vita dhidi ya Wapiganaji wa itikadi kali, rushwa na utawala mbovu kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu katika kuimarisha usalama, uwajibikaji na utendaji wa Serikali.















