Mamlaka nchini Afrika Kusini zimeshtumu vurugu za eneo la Eastern Cape na kutoa wito wa utulivu kufuatia utata wa kusimikwa kwa kiongozi wa kifalme wa Nigeria, jambo lililosababisha taharuki kati ya jamii ya eneo hilo na raia wa kigeni.
Naibu Waziri wa Utawala Bora na Masuala ya Kijadi, Prince Zolile Burns-Ncamashe, alishtumu vurugu hizo mjini KuGompo siku ya Jumatatu, ambapo waandamanaji walichoma moto magari na kupora maduka yanayodaiwa kumilikiuwa na na raia wa kigeni.
Aliomba kuwe na utulivu na kuthibitisha kuwa juhudi za kidiplomasia zinaendelea kufuatia tukio hilo lilohusisha raia wa Nigeria.
Vurugu zimefuatia maandamano dhidi ya taarifa za kusimikwa kwa Mnigeria aliyepewa cheo cha kiongozi wa kijadi wa jamii ya Igbo.
Video zilizosambazwa zinaonesha sherehe hizo, zinazosemekana kufanyika Machi 14, 2026.
Cheo hicho cha “Igwe,” ambacho kinatambuliwa na jamii za Waigbo nchini Nigeria, siyo sehemu ya mfumo wa uongozi wa kijadi nchini Afrika Kusini, ambapo wadhifa kama huo unarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, na kuidhinishwa na mamlaka za kijadi, pamoja na serikali.
Katika ujumbe wa onyo Jumatatu jioni, ubalozi ulitoa wito kwa Wanigeria nchini Afrika Kusini kuwa makini, kutojitokeza sana, na kuepuka mikusanyiko mikubwa, pamoja kutosafiri isipokuwa iwe ni dharura. Pia ulionya kuwa taarifa potofu huenda ikachochea vurugu zaidi, kutatia umoja, na kuzingatia sheria za nchi, pamoja na kuwa raia wema.
Maafisa wa Afrika Kusini pia wamekuwa wakijadiliana na mamlaka za Nigeria, huku Kaimu Balozi wa Nigeria, Alexander AJ Oditah, alinukuliwa akisema kuwa huyo Igwe aliyesimikwa “siyo mfalme na hatambuliwi popote nchini Nigeria.”






