Kundi lenye silaha limewaua watu wasiopungua 20 katika eneo la chuo kikuu kaskazini kati mwa Nigeria katika shambulio la usiku wa manane siku ya Jumapili, kusababisha mamlaka kutangaza marufuku ya kutotoka nje kwa saa 48.
Taarifa za awali kutoka vyombo vya habari vya eneo hilo zimetangaza idadi ya waliouawa kuwa 13, lakini viongozi wa jamii hiyo siku ya Jumatatu walisema idadi ya waliouawa ni watu wasiopungua 20, huku kukiwa na hofu ya idadi kuongezeka zaidi huku juhudi za kuwatafuta watu zikiendelea.
Wakazi na maafisa wa eneo hilo wanasema waliokuwa na silaha walivamia jamii hiyo Jos Kaskazini, Jimbo la Plateau, na kuwafyatulia risasi raia.
Walioshuhudia wanaeleza tukio hilo kuwa taharuki huku milio ya risasi ikisikika, kulazimisha watu kukimbia nyumba zao kwa ajili ya usalama.
Marufuku ya kutotoka nje ya saa arobaini na nane
“Ni masikitiko kuwa wenye silaha wanaendelea kuwashambulia watu wasio na hatia, hii ni hatari sana,” mmoja wa walionusurika aliyejitambulisha kama Steven Enoch aliiambia Anadolu.
Serikali ya Jimbo la Plateau imetangaza marufuku ya saa 48 katika eneo la Jos Kaskazini, kutaka watu wasitoke nje pamoja na kupeleka maafisa wa usalama kutuliza hali na kuzuia vurugu zaidi.
Katika taarifa, Kamishna Habari na Mawasiliano Joyce Lohya Ramnap alisisitiza dhamira ya serikali kulinda maisha ya watu na mali zao, akiapa kuwa wote waliohusika watawajibishwa.
Akishtumu "mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia wasiokuwa na hatia" na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao, Ramnap aliwataka wakazi kuwa watulivu na kujiepusha na mambo ambayo yatazidisha taharuki.
















