Uturuki yafungua kituo cha mafunzo ya upishi kwa wanawake katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Uganda
AFRIKA
3 dk kusoma
Uturuki yafungua kituo cha mafunzo ya upishi kwa wanawake katika Chuo Kikuu cha Kiislamu UgandaKituo kipya cha mafunzo ya upishi kilichofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TİKA) katika Chuo Kikuu cha Kiislamu nchini Uganda (IUIU) kinalenga kuwapatia wasichana ujuzi na kuongeza fursa za ujasiriamali.
Warsha ya kisasa ya sanaa ya upishi itatoa mafunzo ya yenye tija kwa wahitimu wanaojiandaa kuingia katika sekta ya hoteli inayokua nchini Uganda. / / TRT Afrika

Uturuki imeongeza msaada wake kwa elimu ya ufundi nchini Uganda kwa kuzindua Warsha ya Kisasa ya Sanaa ya Upishi na Mafunzo ya Kupika katika Kampasi ya Wanawake ya Chuo Kikuu cha Kiislamu nchini Uganda (IUIU) iliyopo Kabojja, karibu na jiji la Kampala.

Kituo hicho, kilichofadhiliwa na TİKA, kinatarajiwa kuimarisha mafunzo kwa mamia ya wanafunzi wa kike, huku kikikamilisha programu ya ushonaji inayofadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Uturuki, SENA Foundation.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi kituo hicho Alhamisi, Balozi wa Uturuki nchini Uganda, Fatih Ak, amesema mradi huo ni uwekezaji kwa mustakabali wa Uganda, akisisitiza kuwa elimu ya ufundi ina nafasi muhimu katika kuzalisha ajira na kuwawezesha vijana.

"Mradi huu ni zaidi ya uzinduzi wa jengo jipya. Ni uwekezaji kwa watu, elimu na mustakabali wa kizazi cha vijana wa Uganda, hasa wasichana," alisema.

Kuwawezesha watu na uwekezaji katika mustakabali

Ak amesema kuwa katika uchumi wa sasa, ujuzi unazidi kuwa muhimu na unapaswa kuthaminiwa kwa kiwango sawa na elimu rasmi ya kitaaluma.

 "Katika dunia ya leo, elimu ya ufundi ina thamani sawa na elimu ya kitaaluma. Ujuzi huleta fursa, na fursa hubadilisha maisha," alisema.

"Tunatarajia wanafunzi watakaopata mafunzo hapa si tu watajenga taaluma zenye mafanikio, bali pia watakuwa wajasiriamali, watatengeneza ajira kwa wengine na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Uganda."

Balozi huyo alisema warsha hiyo ya upishi ni sehemu ya ushirikiano mpana wa maendeleo kati ya Uturuki na Uganda unaojumuisha sekta za elimu, afya, kilimo, maji na maendeleo ya jamii.

Ushirikiano wa maendeleo

Kwa mujibu wa Ak, TİKA imetekeleza miradi 128 ya maendeleo nchini Uganda kwa kushirikiana na taasisi za Uturuki pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.

"Kila mradi hii unaakisi imani yetu kwamba maendeleo endelevu huanza kwa kuwawezesha watu," alisema.

"Tukisonga mbele, Uturuki itaendelea kujitolea kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo vya Uganda huku ikiimarisha uhusiano wa urafiki, ushirikiano na ustawi wa pamoja kati ya mataifa yetu mawili." 

Kituo hiki kipya cha mafunzo ya upishi pia kinaendeleza mpango uliokuwepo wa mafunzo ya ufundi katika chuo hicho, kwa kupanua fursa kwa wanawake na wasichana kupata ujuzi unaohitajika sokoni ambao unaweza kuwawezesha kupata ajira au kujiajiri.

Mkurugenzi wa Kampasi ya Wanawake ya IUIU, Profesa Mshiriki Dkt. Nabukeera Madinah Ssebyala, alipokea msaada huo kwa furaha, akisema mamia ya wanafunzi watanufaika na kituo hicho kipya.

Alisema warsha hiyo itaimarisha uwezo wa chuo kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya sekta ya ajira na kuwaandaa vyema wahitimu kwa kazi katika sekta inayokua kwa kasi ya huduma za hoteli, magahawa na chakula nchini Uganda.

CHANZO:TRT Afrika