Rais wa Marekani Donald Trump amewasili Beijing kwa mkutano wa ngazi ya juu na kiongozi wa China Xi Jinping unaolenga kupunguza mvutano mkubwa kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani.
Ziara ya Trump ni ya kwanza nchini China kufanywa na rais wa Marekani katika karibu miaka kumi, Trump aliwasili kwa ndege ya Air Force One katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing Capital saa 11:50 GMT Jumatano baada ya safari ndefu kutoka Washington.
Migogoro kuhusu Iran, biashara na Taiwan inatarajiwa kuwa kipaumbele wa mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu kati ya viongozi wa uchumi mkubwa zaidi duniani, ambao Trump alikuwa ameuchelewesha tangu Machi kutokana na vita vya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, Trump alionekana kuelekeza nguvu zaidi kwenye makubaliano ya biashara, huku mfanyabiashara mwenye asili ya Taiwan Jensen Huang akipanda ndege dakika za mwisho huko Alaska na Elon Musk pia akisafiri kwa ndege ya rais.
Wakati ushindani wa kimataifa wa teknolojia ya akili mnemba (AI) ukiendelea kushika kasi, China kwa sasa imepigwa marufuku kununua vifaa vya kielektroniki (chips) za kisasa zinazotengenezwa na Nvidia chini ya sheria za Marekani za usafirishaji nje, ambazo Washington inasema zinalenga kulinda usalama wa taifa.
Trump aliandika katika ujumbe wa mitandao ya kijamii akiwa safarini kwamba “atamwomba Rais Xi, kiongozi mwenye heshima ya kipekee, ‘aifungue’ China ili watu hawa wenye vipaji waweze kuonyesha uwezo wao.”
Akiitembelea China kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017 katika muhula wake wa kwanza, Trump anatarajiwa kupokelewa kwa sherehe kubwa na mamlaka za China na kuwa na ratiba yenye shughuli nyingi.
Trump na Xi watafanya mazungumzo saa 02:00 GMT Alhamisi katika ukumbi wa kifahari wa Great Hall of the People mjini Beijing, ambapo pia watashiriki karamu ya kitaifa jioni hiyo.
Siku ya Ijumaa, wanatarajiwa kunywa chai na kula chakula cha mchana kabla ya Rais Trump Marekani kurejea Marekani.
Alipoondoka Ikulu ya White House, Trump alisema anatarajia kuwa na “mazungumzo marefu” na Xi kuhusu vita vya pamoja vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambayo huuza sehemu kubwa ya mafuta yake yaliyowekewa vikwazo vya Marekani kwa China.
Lakini pia alipunguza uzito wa tofauti zilizopo, akiwaambia waandishi wa habari kwamba “sidhani kama tunahitaji msaada wowote kuhusu Iran” kutoka China na kwamba Xi alikuwa “amekuwa mzuri kiasi” kuhusu suala hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema Jumatano kwamba “inaipongeza” ziara ya Trump na kwamba “China iko tayari kufanya kazi na Marekani… kupanua ushirikiano na kudhibiti tofauti zilizopo.”
‘Makubaliano makubwa’
Hata hivyo, China inaanza kukosa subira kuhusu kupatikana kwa amani, huku Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi akimhimiza mwenzake wa Pakistan Jumanne kuongeza juhudi za upatanishi kati ya Iran na Marekani.
Trump alisema Jumatatu kwamba atazungumza na Xi kuhusu mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan, nchi inayojitawala ambayo China inadai kuwa ni sehemu yake, jambo ambalo ni tofauti na msimamo wa kihistoria wa Marekani wa kutoshirikisha China kuhusu msaada wake kwa kisiwa hicho.
Vita vya biashara vilivyodumu kwa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili pia vitakuwa ajenda kuu, baada ya ushuru mkubwa uliowekwa na Trump mwaka jana kusababisha hatua za kulipizana katika kuongezeana ushuru zilizozidi asilimia 100.
Trump na Xi wanatarajiwa kujadili kuongeza muda wa makubaliano ya kusitisha ushuru kwa mwaka mmoja, ambayo viongozi hao wawili walifikia katika mkutano wao wa mwisho nchini Korea Kusini mwezi Oktoba, ingawa kufikiwa kwa makubaliano mapya bado kunaonekana kuwa jambo lisilo la uhakika.













