Uturuki imekamilisha maandalizi yote kiserikali katika kuanzisha biashara ya moja kwa moja na Armenia ni sehemu ya mchakato unaoendelea wa kurudisha hali kuwa sawa kati ya mataifa hayo mawili, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Oncu Keceli amesema.
Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumanne, Keceli amesema maandalizi yalikamilika Mei 11 kwa misingi ya hatua za kujenga imani zilizochukuliwa tangu mazungumzo ya kurudisha hali kuwa sawa kati ya Uturuki na Armenia kuanza 2022.
Aliongeza kuwa taratibu za kiufundi na kiserikali kwa lengo la kufungua mpaka kati ya nchi hizo mbili zinaendelea.
Chini ya mpango huu mpya, bidhaa zinazosafirishwa kutoka Uturuki hadi Armenia kupitia nchi ya tatu, na kinyume chake, sasa hivi zitaruhusiwa kueleza mzigo unapokwenda au unapotoka kama “Armenia/Uturuki,” Keceli alisema.
Alisema Uturuki itaendelea kuchangia maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi wa mataifa ya Caucasus ya Kusini na kuunga mkono juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa faida za mataifa yote na watu katika kanda.
Tangazo hilo ni la hivi karibuni la hatua za kujenga imani chini ya mchakato wa kurudisha hali kama ilivyokuwa ulioanzishwa tena 2022.
Mwezi Machi, Shirika la ndege la Turkish Airlines lilianzisha safari za kila siku kati ya Istanbul na Yerevan, huku mataifa hayo yakikubaliana kupunguza masharti ya viza kwa wenye hati za kusafiria maalum na za kidilplomasia.
Ujenzi wa mpaka wa Alican-Margara, unaounganisha mkoa wa Uturuki wa Igdir na eneo la Armenia la Armavir, sasa hivi umekamilika kwa asilimia 90.
Hivi karibuni pande zote mbili zimekubaliana kukarabati daraja la kihistoria la Ani lililoko mpakani, ishara nzuri ambayo wanadiplomasia wanasema inaonesha juhudi za kurudisha hali kama ilivyokuwa zamani.
Uturuki na Armenia hawajakuwa na uhusiano rasmi wa kidiplomasia na mpaka wao wa ardhini umefungwa tangu 1993.


















