Huku Kenya ikiendelea kuomboleza vifo vya wanafunzi 16 waliofariki kutokana na moto uliounguza bweni la Shule ya Wasichana ya Utumishi Academy huko Gilgil, baadhi ya wananchi wameonesha hasira na kunyoosheana vidole vya lawama.
Mpaka sasa idadi kamili iliyothibitishwa ya vifo ni 16, lakini kuna wanafunzi 79 ambao walijeruhiwa katika ajali hiyo ya moto iliyotokea Mei 28.
Tayari wanafunzi nane wanashikiliwa na polisi kufuatia uchunguzi wa awali.
Wakati huo huo, mamlaka pia inachunguza madai ya kuwepo kwa msongamano, kufungwa kwa njia za dhararu za kutokea lakini pia, uwezekano wa kuwepo kwa uzembe kutoka uongozi wa shule.
Wasichana waonekana wakiwasha moto
Ajali hii ya moto, inatonesha kidonda cha ajali za moto zilizowahi kutokea shuleni huku suala kubwa likimulikwa katika usalama mzima mashuleni.
Rekodi za serikali zinaonyesha matukio 107 ya moto shuleni kati ya Januari na Septemba 2025 pekee, wakati baadhi ya matukio mabaya zaidi ya moto shuleni yametokea katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo 2024, wanafunzi 21 walifariki kutokana na moto katika bweni la shule ya Hillside Endarasha huko Nyeri. Moto mbaya zaidi wa shule nchini unasalia kuwa janga la Kyanguli la 2001, ambapo wanafunzi 67 walifariki katika tukio la uchomaji moto.
Katika tukio la moto wasichana wa Utumishi Academy, video ya CCTV ilionyesha wasichana wasiopungua 7 wakitembea kwenye moja ya mabweni na wanaonekana wakichoma moto kwenye magodoro na kukimbia nje.
Lawama zinasukumwa pande zote
Video hiyo ya kusikitisha inaendelea kuwaonyesha wasichana wakiamka kwa hofu na kujaribu kukimbia nje huku wengine wakijaribu kuwasaidia wenzao.
Wasichana 4 kati ya 16 waliofariki waliungua kiasi cha kutoweza kutambulika, huku matokeo ya uchunguzi yakionyesha kuwa wote walikufa kutokana na kuungua sana na kukosa hewa.
Wanafunzi 8 waliokamatwa na Kurugenzi ya Upelelezi watafikishwa mahakamani wiki hii kujibu mashtaka ya uchomaji moto, na pengine kuua bila kukusudia na kuua.
Huku hayo yakijiri wengi wameanza kusukumiana lawama kutoka kwa kuwashutumu wazazi kwa kupuuza kuwatia adabu watoto wao, hadi uzembe miongoni mwa wasimamizi wa shule na ukosefu wa utekelezaji wa usalama shuleni.
Shule 15 zimefungwa tangu Mei
Kufuatia wimbi la machafuko na ukaguzi wa usalama, maafisa wa elimu wanasema takriban shule 350 zimefungwa tangu 2024 kwa wasiwasi wa usalama na maswala yanayohusiana na ghasia za wanafunzi.
Kulingana na rekodi za kaunti, angalau shule 15 zimeripoti kusimamishwa kwa masomo na kufungwa kuhusiana na machafuko ya wanafunzi tangu mwanzo wa mwezi Mei.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya moja ya shule hizo, wanafunzi hao walilalamikia sababu nyingi zikiwemo njaa, huduma za afya, ugawi mdogo wa chakula, ukosefu wa ubora wa elimu na jinsi wanafunzi wanavyotendewa na sababu hizo zinaonekana kugusa shule nyingine nyingi.
Bodi mbalimbali za shule zimesema malalamiko hayo tayari yanaangaliwa na kushughulikiwa.
Bodi ya Shule yavunjwa
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen ameamuru kuvunjwa kwa Bodi ya shule ya wasichana ya Utumishi Academy na kupendekeza uchunguzi na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Wasichana hao wanaoshukiwa wamezuiliwa katika seli za polisi kwa siku 3 zilizopita wakisubiri kufikishwa mahakamani wiki hii.















