| Swahili
Maoni
AFRIKA
3 dk kusoma
Kuliondoa Bara la Afrika kutoka kusuasua hadi kutoa muelekeo
Mkutano uliomalizika wa 'Africa Forward Summit' unatakiwa kuonekana kama mwanzo. Lazima tuwe na bara ambalo limejipanga na linafahamu malengo yake kwamba makubaliano ya ushirikiano yameandikwa Nairobi, siyo tu kutiwa saini huko.
Kuliondoa Bara la Afrika kutoka kusuasua hadi kutoa muelekeo
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Kenya William Ruto katika Kongamano la ‘Africa Forward’ 2026 jijini Nairobi, Kenya. /Picha: Reuters

Na Nhial Deng

Mkutano uliomalizika wa Africa Forward Summit jijini Nairobi umeacha vijana wengi wa Afrika kama mimi katika njia panda.

Kwa upande mmoja, Azimio la Nairobi limejaa Uanamajumui, lugha ya kuwa na mustakabali sahihi ambayo wengi walihitaji. Linazungumzia ukuaji wa viwanda, uhuru, na “ushirikiano wa usawa” kati ya Afrika na Ufaransa.

Kwa upande mwingine, kuna hali ya wasiwasi imejitokeza katika mitandao ya kijamii. Wengi wakiangazia historia ya muda mrefu ya Ufaransa ya kuingilia masuala ya nchi katika bara kama sababu ya kuona kongamano hilo halina faida yoyote.

Afrika kwanza?

Kwanza, lazima tuwe wazi kuhusu namna dunia ilivyo. Haijawahi kutokea katika historia uwezekano wa Ufaransa, Marekani, China, au Urusi kuunda sera ya kigeni ambayo inazingatia maslahi ya Afrika. Hiyo siyo diplomasia, na kamwe haitofanyika.

Mwanadiplomasia wa Ufaransa ambaye yuko kwenye majadiiano anaangalia maslahi ya Ufaransa kwanza. Mwanadiplomasia wa China yuko kwa kuzingatia maslahi ya China. Marekani pia ni hivyo hivyo.

Kutarajia taifa la nje kuyapa kipaumbele masuala yetu ya maendeleo kuliko faida zao za kiuchumi ni kutoelewa uhusiano wa kimataifa. Badala ya kudai kuwa mkutano haukuwa sahihi kwa kuwa maslahi ya Afrika hayakuzingatiwa, tunatakiwa kuangazia namna gani tunaweza kubadilisha hali kwa kutumia diplomasia yetu wenyewe.

Mfumo wa kukurupuka

Tatizo la sasa barani Afrika liko liko katika kukurupuka. Tunasubiri nchi zenye uwezo kuweka agenda, alafu tunakurupuka. Ndiyo maana tunahisi tunatengwa.

Njia moja ambayo Afrika inaweza kufanikiwa ni kuwa na sera zake wenyewe za kigeni na mkakati kwanza. Tuondokane na kuwa watu wa kukurupuka tuwe ni wenye kutoa muelekeo. Inabidi tufanyie mabadiliko taasisi zetu wenyewe na tuziimarishe ili tusiitwe kwenye majadiliano kwa lengo la kusaini yaliyoandaliwa tayari. Badala yake, inabidi tuje na mikataba yetu wenyewe mezani.

Azimio la Nairobi linataja umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ule wa fedha kimataifa. Haya ni malengo makubwa, ambayo yanahitaji ushirikiano wa mataifa yenye uwezo ulimwenguni.

Wakati mwanadiplomasia anapokaa kwenye meza moja na mwanasiplomasia wa Ufaransa, jukumu lao linatakiwa kuwa moja. Wanatakiwa kuwa hapo kwa ajili ya maslahi ya Afrika.

Afrika Kwanza

Tunatakiwa kuwa tayari kushirikiana na yoyote ambaye yuko tayari kukubali matakwa yetu. Iwe mshirika anatoka Mashariki au Magharibi, tunatakiwa tufahamu nini hasa wanataka na nini ambacho sisi tutapata.

Kufanikiwa inategemea namba sisi wenyewe tunavyofanya, siyo nani tunashirikiana naye. Kama tunaingia kwenye mikataba hii tukiwa na sera ya kigeni ya uhakika na kwa umoja, tunaweza kufaidika zaidi.

Mkutano wa Africa Forward unatakiwa uonekane kama mwanzo tu. Ni ishara kuwa dunia inatambua umuhimu wetu unaoimarika.

Kama kijana wa Kiafrika, tunatakiwa tusiwe na hofu ya ushirikiano na tuanze kutaka kujuwa kuhusu utekelezaji. Lazima tuwe na bara ambalo limejipanga na linafahamu malengo yake kwamba makubaliano ya uhusiano yameandikwa Nairobi, siyo tu kutiwa saini huko.

Kujadiliana ni kufanikiwa, lakini iwapo sisi ndiyo tunaongoza mazungumzo hayo, na kwa masharti yetu.

Mwandishi, Nhial Deng, ni mshindi wa tuzo kadhaa za ubunifu, msimulizi, na mpanga mikakati wa mifumo ya akili unde, masuala ya kijamii, na uongozi wa vijana.

CHANZO:TRT Afrika