Twiga mweupe pekee duniani anayepatikana nchini Kenya
Twiga mweupe pekee duniani anaishi Kenya/ Picha@AfricanHub / Public domain
Twiga mweupe pekee duniani anayepatikana nchini Kenya
Twiga mweupe pekee duniani wanaishi katika Kaunti ya Garissa, kaskazini-mashariki mwa nchi.

Kupauka kwa twiga hakutokani na ualbino bali ni hali ya nadra ya kijeni inayoitwa ‘leucism’, ambayo huathiri rangi kwenye ngozi lakini si macho.

‘Leucism’ ni hali ya kijenetiki inayosababisha upotevu wa sehemu au jumla wa rangi katika wanyama, na kusababisha ngozi nyeupe, rangi au mabaka, au nywele huku ikibakiza rangi ya kawaida ya macho.

Ualbino kwa upande mwingine unaashiria ukosefu kamili wa melanini au ile rangi ya asili.

Hapo awali kulikuwa na twiga weupe watatu kama hao.

Machi mwaka 2020, walinzi waligundua mabaki ya mifupa ya twiga jike mweupe na ndama wake wa miezi saba katika Kaunti ya Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Walikuwa wameuawa na wawindaji haramu, na wa kiume aliyesalia alikuwa mzao wao wa moja kwa moja.

Wote watatu walikuwa wameishi ndani ya Hifadhi ya Ishaqbini Hirola, eneo linalojulikana kwa juhudi zake za uhifadhi.

Sasa Ili kulinda utajiri huu muhimu wataalam wa wanyamapori waliweka GPS ili kuweza kufuatilia mwenendo wa mnyama huyo Novemba 2020.

GPS inayotumia nguvu za jua imewekwa juu ya kichwa kama pembe.

Twiga yuko huru kuzunguka eneo lake la makazi.

Hata hivyo, iwapo ataelekea katika maeneo yanayoonekana kuwa hatari, kwa mfano kwa wawindaji haramu, kupitia GPS walinzi wanaweza kuchukua hatua haraka na kumtoa kwenye hatari.

GPS hiyo inafuatilia maeneo yake yote ya malisho.

Kabla ya tukio la ujangili, familia ya twiga weupe ilikuwa kivutio kikubwa kwa utalii.

Watalii walisafiri hadi Kaskazini mashariki mwa Kenya ili kujionea wanyama hao adimu.

Na sasa ikiwa amesalia twiga mmoja tu mweupe utalii wa kwenda kumuona mnyama huyo hivi sasa unadhibitiwa.

Aidha kwa kuwa yuko huru kuzurura hata uwezekano wa kumuona kwa urahisi katika hifadhi ni mdogo sana.

CHANZO:TRT Swahili