Kilimo ikolojia kinavyozalisha mamilionea Kaskazini mwa Tanzania
AFRIKA
5 dk kusoma
Kilimo ikolojia kinavyozalisha mamilionea Kaskazini mwa TanzaniaEneo la Karatu linafaidika kwa ukaribu wake na ukanda wa utalii wa kaskazini, unaovutia maelfu ya watalii kila mwaka.
Ndege alipata mafunzo ya kilimo ikolojia kupitia shirika la Iles de Paix yaani Island of Peace (IDP)./Picha:Wengine
tokea masaa 2

Kwenye mteremko mkali unaozungukwa na madhara nzuri ya kijani katika Kijiji cha Yaalabe, wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania, unakutana na bustani iliyopangwa kwa ustadi ya mboga za majani kama vile kabichi na nyinginezo.

Kwa mkulima George Ndege, eneo hili ni ushuhuda wa mageuzi makubwa ya kiuchumi—yanayoakisi mabadiliko mapana katika sekta ya kilimo kaskazini mwa Tanzania.

Miaka minane iliyopita, Ndege alikuwa mkulima wa kujikimu katika kijiji cha Eyalabe, akilima kwa ajili ya chakula cha familia yake pekee.

Leo hii, kilimo hicho cha ikolojia kimegeuka kuwa  biashara yenye faida, akiuza mazao asilia kwenye hoteli za kitalii, na kuingiza mamilioni ya shilingi kila mwaka.

“Sikuwahi kufikiria kilimo kinaweza kunifikisha hapa,” anasema akiwa shambani. “Sasa siioni tena kama njia ya kujikimu tu, bali ni fursa ya kiuchumi.”

Katika shamba lake lenye zaidi ya ekari moja, Ndege amepanda mazao mbalimbali.

Mazao hayo huuzwa kwenye hoteli sita za kifahari katika mji wa Karatu, ambao ni lango kuu la kuingia kwenye vivutio vikubwa vya utalii vya ukanda wa kaskazini mwa Tanzania kama vile Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Kreta ya Ngorongoro.

Kulingana na Ndege, mauzo ya mazao yake, humumhakikishia Dola 68,000 (Shilingi milioni 180) kwa mwaka.

Akijumuisha kipato kutoka shamba lake la kahawa lenye ekari kumi, mapato yake ya mwaka hufikia karibu takribani Dola 100,000 (Shilingi milioni 266), kiwango kisichotarajiwa kwa mkulima mdogo miaka michache iliyopita.

Kilimo kinachobadili uchumi

Mafanikio ya Ndege yanahusishwa moja kwa moja na mafunzo ya kilimo ikolojia (Agroecology) mfumo wa kilimo unaochanganya uzalishaji na uhifadhi wa mazingira, kwa kusisitiza matumizi ya mbegu na pembejeo za asili.

Ndege alipata mafunzo ya kilimo ikolojia kupitia shirika la Iles de Paix yaani Island of Peace (IDP) lenye makao yake makuu jijini Arusha, ambalo limekuwa likifanya kazi na wakulima katika eneo hilo.

“Walitufundisha kutumia tulichonacho—mbegu za asili, na njia za asili za kudhibiti wadudu,” anaeleza. “Hali hii imepunguza gharama na kuongeza mavuno.”

Kupitia ushirikiano na taasisi za ndani kama MVIWArusha na RECODA, IDP imewezesha maelfu ya wakulima kupatiwa mafunzo ya mbinu za kilimo cha ikolojia, wakihamasishwa kulima kwa mtazamo wa kilimo endelevu na kibiashara.

Faida za kiuchumi

Kwa mujibu wa mtaalamu mbobevu wa mifumo ya kilimo Ikolojia wa IDP,  Emmanuel Kasembe, zaidi ya wakulima 6,500 katika wilaya za Karatu na Arusha wanajishughulisha na kilimo endelevu cha ikolojia, kwenye mashamba yenye ukubwa wa ekari 13,000.

Kwa pamoja, wakulima hawa huzalisha maelfu ya tani za vyakula asilia kila mwaka, huku takwimu za IDP zikionesha kuwa mapato ya ujumla kwa mwaka 2025, yalifikia Dola 485,000 (Shilingi bilioni 1.25).

“Hapo awali, kilimo cha kiokolojia kililenga zaidi soko la nje,” anaeleza Mkurugenzi Mkazi wa IDP, Ayesiga Buberwa. “Lakini sasa tunaona mahitaji yakiongezeka ndani ya nchi—watu wanataka chakula salama na cha kuaminika.”

Utalii wachochea soko

Eneo la Karatu linafaidika kwa ukaribu wake na ukanda wa utalii wa kaskazini, unaovutia maelfu ya watalii kila mwaka.

Kuna zaidi ya hoteli za kitalii 140 zinazohudumia wageni wa kimataifa wanaohitaji chakula safi na chenye ubora wa hali ya juu.

Hali hii imefungua soko la uhakika kwa wakulima.

“Mahitaji bado ni makubwa kuliko uzalishaji,” anasema Ndege. “Tunahitaji wakulima zaidi kuingia katika mfumo huu.”

Kwa upande wa serikali za wilaya, hichi  kilimo ni fursa adhimu ya kuchechemua uchumi wa vijijini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Engelbert Aloyce Qorro, anasema mfano wa George Ndege unaonesha wazi mwelekeo mpya wa kilimo.

“Kilimo endelevu si tu kwa ajili ya kulinda mazingira—ni injini ya maendeleo ya kiuchumi,” anasisitiza.

Mwelekeo wa Bara la Afrika

Mwelekeo huu unaonekana pia katika nchi nyingine za Afrika kama Kenya, Uganda na Ethiopia, ambako wakulima wanaotumia mifumo ya kilimo cha ikolojia wameonesha  ongezeko la uzalishaji, ubora wa udongo na mapato.

Mbinu hizi hutegemea zaidi rasilimali za ndani kuliko pembejeo za gharama kubwa, hivyo kuwafanya wakulima wadogo kushiriki kikamilifu katika uchumi.

Kilimo cha kiikolojia  huchochewa na mambo mbalimbali, ikiwemo uelewa wa watu kuhusu aina ya vyakula wanavyohitaji kula kwa ajili ya usalama wa afya zao, na pia soko la kimataifa la vyakula vya asili, linaloendelea kukua na kufikia thamani ya zaidi ya Dola za kimarekani bilioni 220.

Masoko ya ndani barani Afrika nayo yanaongezeka, hasa katika miji na maeneo ya utalii.

 Changamoto zilizopo

 Licha ya mafanikio, bado kuna changamoto kadhaa.

Upatikanaji wa pembejeo za kikaboni zilizoidhinishwa, mitaji, na masoko ya uhakika bado ni vikwazo kwa wakulima wengi.

Aidha, miundombinu duni ya kuhifadhi na kusafirisha mazao inaathiri upanuzi wa biashara.

Mashirika kama Iles de Paix yanaendelea kusaidia kwa kuimarisha mitandao ya wakulima na kuongeza upatikanaji wa rasilimali, lakini wataalamu wanaona umuhimu wa uwekezaji mkubwa zaidi na sera madhubuti za serikali.

Kilimo chenye kubadili maisha

Kwa Ndege, mafanikio haya yameleta mabadiliko makubwa ya maisha. Amejenga nyumba mpya, amewekeza katika vifaa vya kilimo, na ameanzisha biashara ndogo ya hoteli.

Shamba lake sasa linatumika kama kituo cha mafunzo kwa wakulima wengine, hasa vijana.

“Ninawaambia vijana, kilimo ni biashara kama zilivyo nyingine,” anasema. “Ukikifanya kwa weledi, kinaweza kukupa maisha bora.”

Mtazamo wa baadaye

Likiwa limeanzishwa mwaka 1958 na Dominique Pire, shirika la Iles de Paix linaendelea kuhimiza mifumo endelevu ya chakula kwa kushirikiana na jamii za wakulima.

Kaskazini mwa Tanzania, kilimo ikolojia kimeibuka kuwa nyenzo muhimu ya mageuzi ya kiuchumi—ikibadili kilimo kutoka shughuli ya kujikimu kuwa sekta yenye tija na ushindani.

Kadiri changamoto za tabianchi zinavyoongezeka na mahitaji ya chakula salama yakikua, mbinu hii inaweza kuwa suluhisho endelevu—si kwa Tanzania pekee, bali kwa nchi nyingi zinazoendelea duniani.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili