Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anaendelea na ziara yake ya kitaifa ya siku 3 nchini Urusi ambapo amekutana na mwenyeji wake Rais wa Urusi Vladimir Putin na kufanya majadiliano yaliyojikita katika nyanja mbalimbali.
Viongozi hao wawili wamejadiliana ushirikiano wa pamoja katika kilimo, hususan uzalishaji wa mbolea, kilimo cha biashara na uongezaji thamani wa mazao, pamoja na ajira.
Pia wamejadiliana kuhusu teknolojia za kidijitali, mifumo ya serikali mtandao na Akili Mnemba.
Kwa upande wake, Rais Putin amesema katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwa na ongezeko la kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Urusi na kufikia takriban asilimia 20 hadi 25.
Wakati huo huo, Rais Samia anatarajiwa kuongoza jopo la wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi.
Nchi hizo mbili pia zimeingia makubaliano katika sekta ya elimu ambapo mawaziri wa sekta hizo mbili wameshuhudia utiaji saini.
Ziara hii ya Rais Samia nchini Urusi ni ya pili kwa Rais wa Tanzania kufanyika katika kipindi cha zaidi ya nusu karne.
Ziara ya kwanza ilifanyika mwaka 1969 na aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo Julius Nyerere.
Matunda ya ziara hiyo tayari yameanza kuonekana kufuatia taarifa aliyoitowa Msaidizi wa Rais wa Urusi, Yury Ushakov, kwa waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa safari za Shirika la Ndege la Air Tanzania kati ya mji wa kibiashara wa Dar es Salaam na mji mkuu wa Moscow kuanzia Julai 1, 2026.
Alisema kuwa idadi ya watalii wa Urusi wanaotembelea Tanzania inaendelea kuongezeka.
“Msimu huu wa kiangazi, Air Tanzania inapanga kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Moscow,” alisema.
Hii ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na Urusi.




















